Wasiofahamu maana ya kurahisisha biashara wajifunze Morocco na Rwanda- Dkt. Kituyi
Kamati ya biashara na maendeleo ya Umoja wa Mataifa, UNCTAD imesema muarobaini wa biashara barani Afrika kuchangia katika malengo ya maendeleo endelevu, SDGs, ni kwa serikali kupunguza gharama za uagizaji, uzalishaji, usafirishaji pamoja tozo za ushuru zisizo na lazima.
Katibu Mkuu wa UNCTAD, Dkt. Mukhisa Kituyi amesema hayo akihojiwa kwa njia ya simu na Assumpta Massoi wa Idhaa ya Kiswahili ya Umoja wa Mataifa kutoka huko Addis Ababa ambako anashiriki jukwaa la siku tatu la viongozi wa kamati za Afrika za kupunguza gharama za biashara.
Dkt. Kituyi akaanza kwa kutoa mfano ambako kupunguzwa kwa gharama kumeleta nuru akisem, “kutoka bidhaa bandarini, Morocco, imepiga hatua ya maana sana mpaka imefikia kiwango kwamba biashara kubwa nchi hiyo ni kuuza magari, magari yanatengenezwa Morocco, kwa sababu yanafika na kupita baharin kwa urahisi..”
Katibu Mkuu huyo wa UNCTAD akatolea mfano pia Rwanda akisema kuwa, “ miaka miwili iliyopita ilikuwa inachukua karibu siku 28 hadi 30 kusafirisha kontena moja kutoka Kigali hadi Mombasa, nchini Kenya, leo inachukua siku nne.”
Amesema hatua kama hizo zinanufaisha biashara ya nchi hiyo na inaongeza imani za wafanyabiashara wake kwa waagizaji kutoka mataifa ya nje.
Alipoulizwa kuwa ni kwa nini mataifa ya Afrika hayajifunzi kutoka nchi hizo, Dkt. Kituyi amesema, “kuna mengi ya kuchangia, kwa mfano kama taifa liko ndani ya Afrika na linapitisha biashara kupitia taifa lingine, sharti lile taifa ambako biashara inapitia iwe na será ambazo zinaboresha usafirishaji wa bidhaa.”
Hata hivyo amesema ingawa wanawapatia viongozi hao wa kamati za kitaifa stadi za kurahisisha biashara bado jukumu kubwa ni la viongozi wa kisiasa ili waweze kupitisha maamuzi kama ambayo Morocco na Rwanda wamepitisha.
Mkutano huo wa siku tatu umeandaliwa kwa pamoja na UNCTAD, shirika la biashara duniani, WTO, Benki ya Dunia, Muungano wa Ulaya na shirika la forodha duniani.