Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wakimbizi wa Syria waanza kujirejesha nyumbani taratibu

Mwanamke akiwa akiwa amesimama katika nyumba yake katika viunga vya El Khalideh, mjini Homs Syria. (Machi 2019)
UNHCR/Andrew McConnell
Mwanamke akiwa akiwa amesimama katika nyumba yake katika viunga vya El Khalideh, mjini Homs Syria. (Machi 2019)

Wakimbizi wa Syria waanza kujirejesha nyumbani taratibu

Wahamiaji na Wakimbizi

Nchini Syria baadhi ya wananchi waliokimbia makazi yao kutokana na vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyodumu kwa miaka nane sasa, wameanza kurejea kwenye mapagala yao ingawa kazi ya  ujenzi mpya inasalia kuwa na changamoto kubwa.

Miongoni mwa waliorejea kwenye mji wa Homs ni Jihad, ambaye kabla ya kuondoka nyumbani kwake Homs alikuwa anamiliki mamia ya njiwa lakini sasa wamesalia 40 tu.

Jihad amerejea mwaka mmoja uliopita, nyumba yake ni pagala, haina milango, madirisha wala mlango wa mbele, kulala kwao ni kwenye matandiko na hana chochote lakini bado wana nia ya kuishi hapa.

 “Hata kama hauna dari na unasimika hema ndani ya nyumba yako, ni bora hapa kuliko kuishi kwingineko.”

Ukosefu wa utulivu umeathiri pia elimu kwa watoto ambapo Abdelrahman, mtoto wa Jihad hajaenda shule kwa miaka mitatu sasa akisema kila ahamiapo akianza kusoma tu mwezi mmoja, wanahama kutokana na ghasia lakini sasa wamerejea nyumbani.

Uharibifu katika mji wa Homs, Mashariki mwa Syria. Syria ni nchi isiyo na amani zaidi duniani
UNICEF/Penttila
Uharibifu katika mji wa Homs, Mashariki mwa Syria. Syria ni nchi isiyo na amani zaidi duniani

Hivi sasa Jihad na familia yake wanatarajia kukarabati nyumba yao ambapo shirika moja la kiraia limewawekea milango na madirisha kiasi cha kuwezesha njiwa kurejea.

“Katu sitokubali kuuza nyumba yangu ili kupata dunia nzima.”

Hadi mwezi Disemba mwaka jana wakimbizi wa ndani milioni 1.4 nchini Syria wamerejea nyumbani kwa mipango yao wenyewe pamoja na wale walioko ugenini kutokana na machafuko kupungua kwenye maeneo yao.

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, UNHCR limesema linatarajia idadi ya wakimbizi wanaorejea wenyewe kuongezeka mwaka 2019 na linaendelea kusaidia mahitaji ya wakimbizi wa ndani na wale wanaorejea.

Katika miaka nane ya vita vya Syria, zaidi ya raia milioni 6.2 wamekuwa wakimbizi wa  ndani.