Takriban watoto 900 waachiliwa huru na makundi yenye silaha Nigeria:

10 Mei 2019

Watoto takriban 900 waliokuwa wakishikiliwa na makundi mbalimbali yenye silaha Kaskazini Mashariki mwa Nigeria wameachiliwa huru na makundi mbalimbali yenye silaha na kufanya idadi ya walioachiliwa na makundi hayo tangu mwaka 2017 kufikia zaidi ya 1700. 

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo na shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia Watoto UNICEF , jumla ya watoto 894 wakiwemo wasichana 106 wameachiliwa leo na kundi la Civilian Joint Task Force, CJTF , eneo la Maiduguri Kaskazini Mashariki mwa Nigeria kama sehemu ya juhudi na ahadi zake za kukomesha na kuzuia watoto kuingizwa na kutumiwa jeshini.

CJTF ni kundi la wanamgambo linalosaidia majeshi ya ulinzi ya Nigeria kupambana na wanamgambo katika eneo hilo la Kaskazini Mashariki . 

Lilianzishwa mwa 2013 kwa lengo la kuzilinda jamii dhidi ya mashambulizi.

UNICEF inasema kila ahadi inayotekelezwa kwa watoto ambayo inaenda sanjari na matendo ni hatua inayokwenda sahihi kwa ajili ya ulinzi wa watoto na ni muhimu ikatambuliwa na kuchagizwa. 

Akizungumza na waandishi wa habari mjini Geneva Uswisi msemaji wa UNICEF Christopher Boulerac amesema“watoto na vijana walioachiliwa leo watafaidika na programu ya  kuwasaidia kurejea katika maisha  ya kiraia na kupata fursa mpya kwa ajili ya maendeleo yao. Bila msaada huu watoto wengi wanaochiliwa na vikundi vilivyojihami wanapata shida kurejea katiak maisha ya kiraia kwa sababu wengi wao hawana elimu na hawana stadi za ufundi."

UNICEF imesisitiza kwamba bila msaada watoto hawa wanahangaika kuishi maisha ya kawaida kwani wengi wao hawana elimu wala mafunzo yoyote.

 

 

♦ Kutembelea ukurasa maalum wa COP26 bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter