Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Watoto watatu wakiwemo wawili wa kike walitumika kushambulia huko Borno; UNICEF yalaani

Mtoto wa kike mwenye umri wa miaka 15, akiwa na binti yake ambaye alijifungua baada ya kunajisiwa na wapiganaji wa Boko Haram waliomteka na kumtia ujauzito
UNICEF/UN0118457/
Mtoto wa kike mwenye umri wa miaka 15, akiwa na binti yake ambaye alijifungua baada ya kunajisiwa na wapiganaji wa Boko Haram waliomteka na kumtia ujauzito

Watoto watatu wakiwemo wawili wa kike walitumika kushambulia huko Borno; UNICEF yalaani

Amani na Usalama

Imebainika kuwa katika mashambulio ya leo huko Borno nchini Nigeria, watoto watatu, wawili kati yao wasichana, walivalishwa mabomu ili wajilipue kutekeleza mashambulizi hayo yaliyosababisha vifo vya watu 30 na majeruhi 40.

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF limelaani kitendo hicho likisema katu watoto hawapaswi kuwa mabomu ya mwili au kuwa na dhima yoyote kwenye maeneo ya mizozo kaskazini-mashariki mwa Nigeria.

Mwakilishi wa UNICEF nchini Nigeria, Peter Hawkins, amenukuliwa na taarifa iliyotolewa na shirika hilo hii leo mjini Abuja akituma salamu za rambirambi kwa familia za waliouawa huku akiwatia ahueni ya haraka majeruhi.

Bwana Hawkins amesema, “hii haikubaliki kabisa watoto kutumiwa katika nchi hii,” akiongeza kuwa “UNICEF inatoa wito kwa wale wote wanaohusika kwenye mzozo huo walinde watoto wakati wowote na wawaepushe na madhara.”

Kwa mujibu wa Hawkins, tukio la leo linafanya idadi ya watoto walioripotiwa kutumiwa kuvaa mabomu na kujilipua tangu mwezi Januari mwaka huu ifikie watano. Mwaka 2018 jumla watoto 48, wakiwemo wasichana 38 walitumiwa kwenye mashambulizi ya kujilipua.

“Tunatoa wito wetu tena kwa pande husika kwenye mzozo kaskazini-mashariki mwa Nigeria wasitishe haraka mashambulizi dhidi ya raia, waache kutumia watoto kwenye mzozo huu na wazingatie sheria na wajibu wao kwa mujibu wa sheria za kimataifa za kibinadamu,” ametamatisha Bwana Hawkins.

Tangu mwaka 2012, vikundi vilivyojihami huko Kaskazini-mashariki mwa Nigeria vimekuwa vikitumikisha watoto kama wapiganaji, vimebaka na kulazimisha watoto wa kike kuolewa. Baadhi ya watoto hao wa kike wamepata ujauzito na wamejifungua watoto hao bila usimamizi wowote wa mhudumu wa afya.