Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Njaa yaendelea kuizogoma Afrika ya Kaskazini na Mashariki ya Kati:FAO

Mtoto huyu pichani mwenye umri wa miezi miwili ni mkazi wa Hajjah, nchini Yemen na ana unyafuzi. Mzozo unaoendelea nchini Yemen unasababisha mamilioni ya watu wawe hatarini kukumbwa na baa la njaa.
WFP/Marco Frattini
Mtoto huyu pichani mwenye umri wa miezi miwili ni mkazi wa Hajjah, nchini Yemen na ana unyafuzi. Mzozo unaoendelea nchini Yemen unasababisha mamilioni ya watu wawe hatarini kukumbwa na baa la njaa.

Njaa yaendelea kuizogoma Afrika ya Kaskazini na Mashariki ya Kati:FAO

Malengo ya Maendeleo Endelevu

Tatizo la njaa linaendelea kuongezeka katika ukanda wa Mashariki ya Kati na Afrika ya Kaskazini (NENA) ambako watu milioni 52 wanakabiliwa na lishe duni na utapiamlio , imesema leo ripoti ya shirika la chakula na kilimo FAO.

Kwa mujibu wa shirika la FAO,  vita, kuongezeka kwa pengo baina ya vijijini na mijini na migogoro ya muda mrefu ambayo inasambaa na kuzidi kuwa mibaya tangu mwaka 2011, vinatishia juhudi za ukanda huo kufikia ajenda ya maendeleo endelevu ya mwaka 2030 ikiwemo kutokomeza njaa.

Ripoti iliyochapishwa leo na FAO ambayo ni ya “Mtazamo wa kikanda kuhusu uhakika wa chakula na lishe” inaonyesha kuwa watu milioni 52 katika ukanda huo wanasumbuliwa na lishe duni na utapiamlo.

Ripoti inasema vita ndio chachu kubwa ya njaa katika ukanda huo huku watu zaidi ya theluthi mbili wanaokabiliwa na njaa katika ukanda wa NENA ambao ni takriban milioni 34, wanaishi katika nchi zilizoghubikwa na vita, ukilinganisha na watu milioni 18 katika nchi ambazo hazijaathirika moja kwa moja na migogoro.

Sababu kubwa

Kwa mujibu wa ripoti hiyo Kudumaa, kula na lishe duni ni tatizo kubwa zaidi katika maeneo yenye vita kuliko katika nchi zingine. Akiongezea hapo Abdessalam Ould mkurugenzi msaidizi wa FAO na mwakilishi wa kikanda (NENA) amesema “Vita na kutokuwepo na utulivu kwa raia kuna athari za muda mrefu katika masuala ya chakula na uhakika wa lishe kwa nchi ziliazoathirika na vita na kwa nchi jirani katika ukanda mzima.Na athari za vita zimevuruga uzalishaji wa chakula na mifugo katika baadhi ya nchi na kuathiri vibaya upatikanaji wa chakula na lishe katika ukanda mzima.”

Ameongeza kuwa kuongezeka kwa tatizo la njaa pia kunachangiwa na ukuaji wa haraka wa idadi ya watu , rasilimali haba, maliasilia haba, ongezeko la tishio la mabadiliko ya tabianchi, kuongezeka kwa atatizo la ajira, kupungua kwa uzalishaji wa kilimo na miundombinu hafifu na ukosefu wa huduma za msingi vijijini.

 

Utupaji hovyo wa chakula ni adui mkubwa wa vita dhidi ya njaa
FAO/Jonathan Bloom
Utupaji hovyo wa chakula ni adui mkubwa wa vita dhidi ya njaa

 Matatizo mengine

Ripoti imeainisha kwamba ukanda huo mbali ya njaa unakabiliwa pia na changamoto zingine ikiwemo kiwango kikubwa cha utipwatipwa au unene wa kupindukia hali ambayo inaongeza shinikizo katika afya za watu, mfumo wa maisha, mifumo ya afya na uchumi wa ukanda huo.

Ripoti inasema ili kushughulikia matatizo ya utipwatipwa kunahitajika mifumo ya chakula ambayo itahakikisha kwamba watu wana fursa ya lishe bora na kuongeza ulelewa miongoni mwa jamii , lakini pia tarifa za kuhusu hatari zinazotokana na hali ya utipwatipwa na uzito wa kupindukia.

Suala lingine lililoainishwa na ripoti hiyo ni kutokuwepo na mabadiliko yanayostahili vijijini ambayo ni moja ya sababu inayochangia kuzorotesha juhudi za kutokomeza njaa na utapiamlo.

Imesisitiza kuwa migogoro mbali ya kuathiri juhudi za kutokomeza njaa lakini pia inaendelea kudunisha maendeleo ya vijijini na mabadiliko yanayohitajika.

Mtoto Fawz anayeugua utapiamlo uliokithiri akipatiwa huduma kwenye hospitali ya Aden nchini Yemen Novemba 2018
OCHA/Giles Clarke
Mtoto Fawz anayeugua utapiamlo uliokithiri akipatiwa huduma kwenye hospitali ya Aden nchini Yemen Novemba 2018

Mabadiliko katika kilimo kufikia lengo

Katika ngazi ya kikanda ripoti inasema kuna fursa kubwa kwa ajili ya kuleta mabadiliko ya kilimo katika njia endelevu, kuanzia na kuborewsha upatikanaji wa masoko kwa ajili ya wakulima, kuchagiza uwekezaji katika kilimo, kuhamishia teknolojia inayohitajika, utendaji sanifu na usimamizi mzuri wa rasilimali ya maji , mabadiliko ya será muhimu ambazo zinasaidia kuleta mabadiliko kutoka kilimo cha chakula tu na kuingia katika kilimo cha biashara na mifumo ya uzalishaji wa mazao tofauti.

FAO inasema ni muhimu kuwachagiza wakulima katika ukanda huo kuzalisha kutokana na mahitaji na soko katika kanda hii italeta faida kwao na ukanda mzima.

Shirika hilo limeongeza kuwa ukanda wa NENA una uwezekano mkubwa katika uzalishaji wa mazao na mifugo ambayo inavumilia hali ya hewa n ya ukanda huo. Hivyo ripoti imesisitiza kuchukuliwa kwa hatua muafaka ili kusaidia kufikia azma ya maendeleo ya kikanda  na utekelezaji wa kuziba pengo kubwa lililopo baina na mijini na vijijini .