Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Choo kimoja watu 200 Ghouta Mashariki

Raia wakiwemo watoto wasubiri msaada wa kibinadamu iwasilishwe na UNICEF chama cha Red Crescent wa kiarabu huko Ghouta Mashariki.
© UNICEF/UN0162765/Al-Mohibany
Raia wakiwemo watoto wasubiri msaada wa kibinadamu iwasilishwe na UNICEF chama cha Red Crescent wa kiarabu huko Ghouta Mashariki.

Choo kimoja watu 200 Ghouta Mashariki

Amani na Usalama

Choo kimoja kutumiwa na watu 200, gharama ya yai moja ni dola 4, mfuko mmoja wa mkate dola 4, ni simulizi kutoka kwa wakimbizi walioweza kukimbia kutoka eneo la Ghouta Mashariki nchini Syria.

Ni katika eneo hilo ambako makombora yanaendelea kuporomoshwa mfululizo licha ya azimio la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa la kutaka sitisho la mapigano ili huduma ziwafikie walengwa.

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF linasema kuwa kutokana na hali hiyio raia wengi wa Syria wameendelea kukimbia eneo hilo na wanahahifadhiwa kwenye vituo vinne vilivyo eneo la Harjeleh.

Hata hivyo hadi sasa hawana taarifa sahihi kuhusu hali ilivyo huko Ghouta ambako hawajaweza kuingia zaidi ya kupata simulizi kutoka kwa wakimbizi.

Ingawa hivyo UNICEF imefika kwenye vituo vya kuwahifadhi na kuwapatia huduma muhimu ikiwemo maji, vifaa vya kusitiri watoto na vile vya kujisafi.

Baba aliamua kumbebea mwanae kwenye sanduku baada ya kupata ruhusu ya kuondoka Ghouta Mashariki kupitia eneo la Hamourieh tarehe 15 Machi, 2018
© UNICEF/UN0185401/Sanadiki
Baba aliamua kumbebea mwanae kwenye sanduku baada ya kupata ruhusu ya kuondoka Ghouta Mashariki kupitia eneo la Hamourieh tarehe 15 Machi, 2018

Picha za wakimbizi hao wakiwa katika harakati za kukimbia Ghouta Mashariki zinawaonyesha wakiwa na huzuni huku baba mmoja akiwa amembeba mtoto wake kwenye sanduku, mtoto akionekana akiwa amechoka.

Geert Cappelaere, ni mkurugenzi wa UNICEF kanda ya Masharikiya Kati na Afrika Kaskazini.

(Sauti ya Geert Cappelaere)

“Karibu asilimia 40 ya watoto kutoka Mashariki ya Ghouta wanakabiliwa na utapiamlo uliokithiri, hii ni dalili dhahiri ya hali mbaya ya afya ya watoto. Na hata hatuzungumzia athari ya kisaikolojia kwa watoto kwa sababu machungu waliyopitia, wakishuhudia wanafamilia na marafiki zao wakiuawa. Wamekuwa wanaishi kwenye mahandaki chini kwa saa kadhaa usiku na mchana. Athari waliyopata watoto bado haijatathminiwa.”

Wanawake na watoto wao wakiwa na virago vyao baada ya kupata fursa ya kuweza kukimbia Ghouta Mashariki kupitia eneo la Hamourieh tarehe 15 Machi 2018.
UNICEF/UN0185408/Sanadiki
Wanawake na watoto wao wakiwa na virago vyao baada ya kupata fursa ya kuweza kukimbia Ghouta Mashariki kupitia eneo la Hamourieh tarehe 15 Machi 2018.

Bwana Cappelaere amenukuu ujumbe wa watoto wa Syria kwa wajumbe wa Baraza la Usalama au yeyote mwenye ushawishi kwa pande kinzani Syria akisema..

(Sauti ya Geert Cappelaere)

“Kwa wale mnaoketi kwenye Baraza la Usalama bado hamjachelewa au kwa wale mlio na ushawishi pande zinazopigana nchini Syria. Katu hakuna kuchelewa kuanza kuheshimu haki za watoto kuhakikisha kila haki ya mvulana na msichana inalindwa.”