Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ulinzi wa haki ya mtoto ni msingi wa mafanikio ya mkataba wa amani CAR- Gamba

Watoto hawa zamani walikuwa wametumikishwa na vikundi vilivyojihami, hivi sasa wamejisalimisha na wako kwenye kambi ya Elevage huko Bambari nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati, CAR
UNICEF/Ashley Gilbertson
Watoto hawa zamani walikuwa wametumikishwa na vikundi vilivyojihami, hivi sasa wamejisalimisha na wako kwenye kambi ya Elevage huko Bambari nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati, CAR

Ulinzi wa haki ya mtoto ni msingi wa mafanikio ya mkataba wa amani CAR- Gamba

Amani na Usalama

Mwakilishi maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kwa ajili ya watoto kwenye mizozo, Virginia Gamba amehitimisha ziara  yake huko Jamhuri ya Afrika ya Kati, CAR akisema usaidizi madhubuti kwa wavulana na wasichana walioathirika na mzozo nchini humo ni jawabu mujarabu la kufanikisha mkataba wa amani uliotiwa saini mwezi Februari mwaka huu. 

Bi. Gamba aliwasili Jamhuri ya Afrika ya Kati kwa ziara ya siku tano kufuatia mwaliko wa Rais Faustin Archange Touadéra.

Alikuwa na mazungumzo na Rais Touadéra na viongozi wengine akiwemo Waziri Mkuu na Rais wa Bunge la nchi hiyo pamoja na vikundi vilivyojihami ambavyo vilitia saini makubaliano ya amani, viongozi wa dini, mabalozi na wawakilishi wa mashirika ya kiraia.

Alitembelea miji ya Bangui na Kaga Bandoro ambako alikutana na watoto ambao awali walitumikishwa vitani lakini sasa wanapatiwa mafunzo stadi ikiwemo umakenika, utengenezaji wa pampu na uoakaji mikate.

Jospin (katikati) mkimbizi wa ndani wakiwa kwenye darasa linaloendelshwa na Ujumbe wa Umoja wa Mataifa, CAR, MINUSCA.
UNICEF/UN0149422/Sokhin
Jospin (katikati) mkimbizi wa ndani wakiwa kwenye darasa linaloendelshwa na Ujumbe wa Umoja wa Mataifa, CAR, MINUSCA.

Kituo hicho cha Don Bosco kinaendeshwa kwa ubia baina ya shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF, Don Bosco na Intersos, ambapo mkurugenzi wa kituo hicho Kevin Kouhalama amesema,“tuna ubia wa kufanya kazi na UNICEF, tunafanya mambo mengi katika masuala ya watoto na kwa hiyo leo kile kilichomleta ni mradi wa maji ambao wamefadhili. Amekuja kuona tumefanyaje uchimbaji na vitu vingine vya mradi huo.”

Na baada ya kujionea hali halisi kuzindua kampeni ya chukua hatua kulinda watoto walioathiriwa na mizozo pamoja na kuepusha ukatili dhidi ya watoto kwa mujibu wa azimio bamba 2427 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, Bi. Gamba amesema, “kwa mkataba wa amani uliotiwa saini mwezi Februari, Jamhuri ya Afrika ya Kati iko katika mwelekeo mpya na moja  ya  ujumbe niliotoa wakati wa ziara yangu ya sasa na zijazo ni kwamba ni lazima kuhakikisha ulinz iwa watoto na barubaru wote wa Jamhuri ya Afrika ya Kati na kuzuia ukiukwaji wa haki zao. Hii ni muhimu sana katika kujenga amani ya kudumu. Ujumbe huo ndio msingi wa kampeni yetu mpya ya kulinda watoto kwenye mizozo.”