Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Chukua hatua kuwalinda watoto walioathiriwa na mgogoro-Virginia Gamba

Mwakilishi wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kwa ajili ya watoto na migogoro ya silaha Bi Virginia Gamba akipokelewa na Waziri mambo ya nje wa Mali katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Bamako Mali.
MINUSMA
Mwakilishi wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kwa ajili ya watoto na migogoro ya silaha Bi Virginia Gamba akipokelewa na Waziri mambo ya nje wa Mali katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Bamako Mali.

Chukua hatua kuwalinda watoto walioathiriwa na mgogoro-Virginia Gamba

Amani na Usalama

Mwakilishi wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kwa ajili ya watoto na migogoro ya silaha Bi Virginia Gamba yuko ziarani nchini Mali na ametembelea mji wa Mopti kujadiliana na wadau kuhusu masuala yanayohusiana na watoto walioathiriwa na mgogoro.

Bi Gamba ameambatana na naibu mwakilishi maalumu wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini Mali ambaye pia ni Kiongozi wa mpito wa ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kuweka utulivu Mali, MINUSMA, Joanne Adamson, na pia mwakilishi mkazi wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF nchini humo, Lucia Elmi.

Baada ya taarifa fupi kutoka kwa kaimu kiongozi wa ofisi ya MINUSMA mjini Mopti Brou Djekou, Bi Gamba, Adamson na Elmi wakakutana na mkuu wa baraza la mawaziri la eneo hilo.

Viongozi hao wa Umoja wa Mataifa pia wamekutana na watoto ambao wameathirika na mgogoro wakiwemo wavulana na wasichana ambao awali walihusishwa na makundi yenye silaha na kisha wakarejea katika jamii zao. Bi Gamba akasema,

(Sauti ya Virginia Gamba)

“Niko hapa Mopti kwasababu tumekuwa na hofu kuhusu kuongezeka kwa vurugu dhidi ya watoto hususani kupitia vurugu za kati ya jamii na jamii. Tumeongea pia na kiongozi wa wafanyakazi katika utawala wa hapa Mopti na tumetaka kuona matokeo ya makubaliano mapya kati ya pande mbili ambazo zinapigana, kuona namna ya kudhibiti vurugu dhidi ya watoto na tutaendelea kujikita na hili. Nimetaka pia kusikia moja kwa moja kutoka kwa watoto walioathirika na vurugu hizi katika eneo hili, wanachofikiria kuhusu vurugu na namna wanavyotaka kutoka katika hali hiyo na mawazo gani kuhusu kuchangamana wanakokutaka. Kwa hivyo, kiujumla tuna hofu lakini tuna tumai kuwa kwa hatua sahihi na kusikiliza kile watoto wanachokitaka, tunaweza kufanikiwa kusitisha na kuzuia ukiukwaji dhidi ya watoto.”

Kabla ya kuondoka Mopti, wajumbe wamebadilishana mawazo na watetezi wa masuala ya utu na viongozi wa jamii za Peuhl na Dogon. Kwa washiriki wote, Bi Gamba amerejelea wito wa umuhimu wa kuwalinda watoto hususani wakati wa migogoro lakini pia umuhimu wa kuwarejesha katika jamii watoto waliokuwa wapiganaji, hiyo ikiwa ni katika utekelezaji wa makubaliano ya amani.

Anaporejea mjini Bamako, Bi Virginia Gamba anatarajiwa kuendelea na mikutano kadhaa na mamlaka za Mali na wadau wengine wa mchakato wa amani, pia atazindua mkakati wake mpya uliopewa jina “Chukua hatua kuwalinda watoto walioathiwa na mgogoro.”