Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Miradi ya MINUSCA ya matokeo ya mapema yaleta matumaini kwa wakazi wa Kaga Bandoro

Daraja hili la Sérébanda lililopo kwenye mji mkuu wa jimbo la Nana Gribizi, Kaga Bandoro nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati, CAR , linakarabatiwa na MINUSCA kama moja ya miradi yake ya matokeo ya haraka ya kuleta amani na kuimarisha kipato.
MINUSCA Video
Daraja hili la Sérébanda lililopo kwenye mji mkuu wa jimbo la Nana Gribizi, Kaga Bandoro nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati, CAR , linakarabatiwa na MINUSCA kama moja ya miradi yake ya matokeo ya haraka ya kuleta amani na kuimarisha kipato.

Miradi ya MINUSCA ya matokeo ya mapema yaleta matumaini kwa wakazi wa Kaga Bandoro

Amani na Usalama

Nchini Jamhuri ya Afrika  ya Kati, CAR ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kuweka utulivu, MINUSCA unajenga daraja ambalo litasaidia siyo tu usafiri bali pia kuleta amani kwenye eneo la kaskazini mwa nchi hiyo.

MINUSCA inakarabati daraja hilo la zamani linalopita kwenye mto Nana kwenye mji wa Kaga Bandoro ambao ni mji mkuu wa jimbo la Nana Gribizi lililoko kaskazini mwa Jamhuri ya Afrika ya Kati, CAR.

Daraja hili liitwalo Sérébanda, ukarabati wake ni kupitia miradi ya matokeo ya haraka ya MINUSCA au QIP ambayo pamoja na kusaidia kuimarisha amani lakini pia inaboresha miundombinu na kusaidia wananchi kuongeza kipato pale walipo.

Raphael Gantada ambaye ni mratibu wa misaada MINUSCA anasema daraja hilo ni muhimu sana kwa sababu, "linaunganisha wilaya mbili na kuna soko lipo upande wa pili. Na kila wakati kuna magari yanapita hapa kueleka Bangui na pia mifugo inapitishwa na kadhalika. Kwa hiyo basi linaunganisha miji ya Nana Gribizi. Hivi karibuni kulikuwepo na wito wa  usaidizi kutoka kwa wafanyabiashara na wananchi wenyewe na ndipo MINUSCA ikaamua kukarabati hili daraja ili kurahisisha usafirishaji na wakati huo huo kulinda raia. “

Hatua hii ya MINUSCA inaungwa mkono na wananchi na miongoni mwao ni Moussa DieuDonné mkazi wa Kaga Bandoro ambaye anasema kwamba “ni barabara kubwa, inayoenda mpaka Bamibawe, hadi hata Sudan. Lakini MINUSCA imefanya mbio kumaliza kazi, raia walikuwa wanateseka . Mimi mwenyewe ni msukuma mkokoteni.”

Ukarabati wa daraja la Sérébanda utasaidia kuimarisha mamlaka za taifa na pia maeneo ya ndani ya mji wa Kaga Bandoro ambapo meya wa mji huo ameongeza pia utasaidia kupunguza ajali ambazo zimekuwa zikitokea mara kwa mara.