Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Tunahitaji dunia isiyo na vifo na majeruhi wa ajali za barabarani:WHO

Ajali za barabarani yatajwa kuwa sababu kuu ya vifo vya vijana
UN News
Ajali za barabarani yatajwa kuwa sababu kuu ya vifo vya vijana

Tunahitaji dunia isiyo na vifo na majeruhi wa ajali za barabarani:WHO

Malengo ya Maendeleo Endelevu

Maadhimisho ya tano ya kimataifa ya wiki ya Umoja wa Mataifa ya usalama barabarani yameanza leo na maelfu ya wanaharakati duniani kote wakichagiza haja ya kuwa na uongozi thabiti kwa ajili ya kuokoa na kulinda maisha ya watu barabarani. 

Kwa mujibu wa shirika la afya ulimwenguni WHO licha ya hatua kubwa zilizopigwa vifo vitokanavyo na ajali za barabarani vinaendelea kuongezeka na sasa kufikia vifo milioni 1.35 kwa mwaka, huku majeraha ya ajali hizo ndio chanzo kikuu cha vifo vya watoto na vijana wa umri wa miaka 5-29.

Shirika hilo linasema viongozi imara wa serikali na wasio wa serikali ndio hupaza sauti kwa ajili ya usalama barabarani na kuchukua hatua kukabiliana na hali hiyo ambazo kwa kiasi fulani zimesaidia kuokoa Maisha lakini limetoa wito kwamba hiyo ni kazi ya kila mmoja.

Hata hivyo WHO inasema bado haitoshi na jitihada zaidi zinahitajika kwani “duniani kote vifo vyote vya ajali za barabarani, kwa watembea kwa miguu na waendesha baiskeli ni asilimia 26 na waendesha pikipiki na abiria wanaowabeba ni asilimia 28, na kwamba hatari ya vifo vya ajali za barabarani bado ni mara tatu zaidi katika nchi za kipato cha chini kuliko zile za kipato cha juu , huku kiwango kikubwa kikipatikana barani Afrika ambako watu 26.6 hufa kwa ajali hizo kwa kila watu laki moja na kiwango cha nini kikiwa barani Ulaya .

Kaulimbiu ya mwaka huu katika wiki ya usalama barabarani itakayoisha Mei 12 ni #Paza sauti kwa ajili ya usalama barabarani” na mkurugenzi mkuu wa WHO Dkt. Tedross Adhanom Ghebreyesus amesisitiza kuwa lengo la shirika hilo ni “kuwa na dunia huru bila vifo wala majeruhi wa ajali za barabarani na pia kuwa na dunia ambayo watu wote wanafaidika na huduma za afya ikiwemo za msaada wa kisaikolojia kwa wagonjwa mahututi, majeruhi na msaada kwa manusura. .

Pia amesisitiza kwamba kampeni hii ya #paza sauti kwa ajili ya usalama barabarani lengo lake ni kuhakikisha watu wasisikia kila wakati athari na ajali hizo ikiwemo mzigo wanaoubeba wanaoacha na wale waliojeruhiwa na kupoteza viungo au kushindwa kufanya lolote na kusalia tegemezi maisha yao yote, jambo ambalo anaamini lisasaidia kupunguza ajali hizo hasa miongoni mwa vijana.

Ameongeza kuwa “Vifo na kujeruhiwa bararabani ni gharama ambayo hakuna anayestahili kuibeba na hakuna msamaha kwa kutochukua hatua dhidi ya unywaji pombe na kisha kuendesha magari, kwenda kasi kupita kiasi na kutovaa mikanda.