Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Watu 3,400 hufa kila siku kwa ajali za barabarani:WHO

Magari yakiwa katika msongamano katikati ya mji wa Monrovia nchini Liberia (Januari 2018)
Picha na UN/Albert González Farran
Magari yakiwa katika msongamano katikati ya mji wa Monrovia nchini Liberia (Januari 2018)

Watu 3,400 hufa kila siku kwa ajali za barabarani:WHO

Malengo ya Maendeleo Endelevu

 Kila siku ajali za barabarani hukatili uhai wa maelfu ya watu, kuwaacha wengine na ulemavu wa maisha na kuathiri mustakhbali wa familia nyingi duniani. Na wakati wa kuchukua hatua dhidi ya zahma hiyo ni sasa limesema shirika la afya duniani, WHO.

Katika taarifa yake ya siku ya kuwakumbuka waathirika wa ajali za barabarani hii leo , WHO imesema maisha ya watu milioni 5 yanaweza kuokolewa katika muongo wa “Hatua kwa ajili ya usalama barabarani ulioanza 2011-2020” likisisitiza kuwa lengo ni kupunguza kwa asilimia 50 majeruhi na vifo vitokanavyo na ajali za barabarani ifikapo 2020 ,  katika juhudi za kutimiza malengo ya maendeleo endelevu au SDG’s hususani lengo la afya namba 3.6.

Kwa mujibu wa takwimu za WHO watu 3,400 hupoteza maisha kila siku kutokana na ajali za barabarani na athari zake kwa familia na jamii kwa ujumla ni kubwa sana, kwani vifo hivyo vya ghafla huacha kovu la milele kwa familia ikiwa ni pamoja na kwa majeruhi katika kila kona ya dunia na huongeza idadi ya mamilioni wanaosalia kuwa tegemezi kwa njia moja au nyingine.

Siku hii pia inalenga kushikamana na mamilioni ya waathirika kote duniani ambao wanataka kutambulika na watu kufahamu madhila yanayowakabili kutokana na ajali hizo.

Image
Maafisa wa usalama barabarani wanapima kiwango cha mwendo kasi barabarani. Picha: UM/Martine Perret

Utafiti wa WHO unaonyesha kuwa asilimia 40-50 ya madereva huendesha kasi zaidi ya kipimo kinachonatakiwa, hali ambayo husababisha ajali moja kati ya tatu zinazotokea barabarani kila siku.

Kwa kutambua umuhimu wa kupunguza ajali hizo, mwezi Aprili mwaka huu Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa liliamua kupitisha hatua kadhaa ili kuchapusha mchakato wa kufikia malengo ya SDG’s yanayohusiana na usalama barabarani. Miongoni mwa hatua hizo ni kukubali pendekezo la serikali ya Sweden kuwa mwenyeji wa mkutano wa tatu wa kimataifa wa ngazi ya juu kuhusu usalama barabarani utakaofanyika 2020, pia makubaliano ya malengo 12 ya kimataifa ya usalama barabarani na kuanzisha wakfu wa Umoja wa Mataifa wa usalama barabarani.

Siku ya kuwakumbuka waathirika wa ajali za barabarani duniani huadhimishwa kila mwaka katika Jumapili ya tatu ya mwezi Novemba kwa ajili ya kuwaenzi mamilioni ya watu waliopoteza maisha na kujeruhiwa katika ajali za barabarani duniani pamoja na familia zao, marafiki na wengine wengi walioathirika kwa njia moja au nyingine kutokana na ajali hizo.