Dawa bandia zaendelea kuleta machungu kwa nchi zinazoendelea
Takribani aina moja ya dawa kati ya 10 zinazotumika katika nchi za kipato cha chini na kati ni bandia au hazijakidhi viwango.
Hii ni kwa mujibu wa utafiti mpya uliotolewa leo na shirika la afya ulimwenguni, WHO.
WHO inasema taarifa hizo zinamaanisha kwamba watu wanatumia dawa ambazo zinashindwa kutibu au kuzuia magonjwa na hiyo haisababishi tu hasara ya kiuchumi bali pia vifo.
Ripoti inalaumu utandawazi ikisema inasababisha mazingira magumu ya kuweka kanuni za kudhibiti utengenezaji wa dawa, ikisema idadi kubwa ya dawa hutengenezwa nchi nyingine na kusafirishwa hadi maeneo mengine kwa ajili ya kufungashwa na kusambazwa.
Akizungumzia utafiti huo, Mkurugenzi Mkuu wa WHO Dkt. Tedros Adhanon Ghebreyesus amesema waathirika zaidi wa dawa hizo ni maskini zaidi akitolea mfano mama ambaye anauza chakula ili anunue dawa kumtibu mwanae, lakini mwishowe mtoto anafariki dunia kwa kuwa dawa haikuwa na nguvu ya kumtibu.
Dkt. Tedros amesema hiyo haikubaliki kwa hivyo nchi lazima zikubaliane juu ya hatua za kuchukua kivitendo kuondokana na tatizo hilo.
Tangu mwaka 2013, WHO imepokea ripoti 1500 za visa vya dawa bandia au zisizokidhi viwango zikiwemo dawa za kutibu malaria na viuavijasumu au antibayotiki.
Asilimia 42 ya visa hivyo ni katika nchi za Afrika zilizo kusini mwa jangwa la Sahara, ikifuatia nwa asilimia 21 Amerika na asilimia 21 ukanda wa Ulaya.