Walibya 42,000 watawanywa na machafuko ya karibuni Tripoli

30 Aprili 2019

Nchini Libya maelfu ya wanawake, watoto na wanaume wamelazimika kufungasha virago na kukimbilia nje ya mji mkuu Tripoli kufuatia machafuko yanayoendelea katika eneo la Kaskazini la mji huo.

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR linasema kwa mujibu wa taarifa zilizopatikana hadi sasa watu 278 wameuawa na wengine 1332 wamejeruhiwa, huku uvurumishaji wa makombora na majibishano makali ya risasi vimesababisha uharibifu mkubwa na kutawanya watu zaidi ya 42,000 huku idadi hiyo ikitarajiwa kuongezeka kutokana na machafuko hayo yaliyoanza mwanzoni mwa mwezi huu wa Aprili.

UNHCR inasema ni muhimu kwa pande zote husika katika mapigano hayo kuhakikisha kwamba raia hawakumbwi katikati ya mapigano na kutoshambulia miundombinu yao. Shirika hilo limeongeza kuwa katika maeneo yaliyoathirika watu wako katika taharuki huku wengine wakioigopa kuziacha nyumba zao.

Mkimbizi kutoka Sudan akisubiri matibabu katika kituo cha afya cha UNHCR Tripoli, Libya
UN OCHA/GILES CLARKE
Mkimbizi kutoka Sudan akisubiri matibabu katika kituo cha afya cha UNHCR Tripoli, Libya

”Kuna upungufu mkubwa wa maji, umeme unakatika mara kwa mara na kuna upungufu mkubwa wa chakula, mafuta na mahitaji mengine ya msingi," limesema shirika hilo likiongeza kuwa  mbali ya kutoa huduma zingine linajaribu kuwalinda wakimbizi na wahamiaji nchini Libya katika mazingira magumu ya sasa, na likiendelea kutoa msaada kwa raia wa Libya walioathirika na machafuko hayo ikiwemo kutoa msaada wa madawa na vifaa tiba kwa wizara ya afya ya Libya wiki hii.

Miongoni vya vifaa hivyo ni magari matatu ya kubeba wagonjwa yaliyokabidhiwa kwa hospitali kuu ya Tripoli, hospitali ya  Hadaba Alkhadra na kwa kituo cha taifa cha maradhi ya moyo cha Tajoura.

UNHCR kwa kushirikiana na mshirika wake Libaid na mashirika mengine ya nchini humo wamefikisha msaada wa mablanketi, magodoro, kandili zinazotumia sola, vifaa vya kupikia, ndoo za kuchotea maji na vifaa vingine muhimu kwa watu 6,200 waliotawwanywa na machafuko ambao sasa wamepatiwa hifadhi katika maenep ya 
Tripoli, Azzawya, Sabratha, Garabulli na Misrata.

Hata hivyo UNHCR inasema kutokana na machafuko yanayoendelea mashirika mengi ya misaada yanashindwa kupata fursa ya kuwafikia waathirika katika baadhi ya maeneo.
Na sasa shirika hilo limetoa wito wa kuruhusu mashirika ya kibinadamu kupata fursa ya kufika katika maeneo yaliyoathirika na kukubali kuwepo kwa usitishaji mapigano kwa muda kuhakikisha huduma za dharura na raia kuweza kuondoka katika maeneo ya vita kwa usalama.

Hali  ya mapigano kwenye mji mkuu wa Libya, Tripoli
UNOCHA
Hali ya mapigano kwenye mji mkuu wa Libya, Tripoli

Usalama wa wahamiaji na wakimbizi Tripoli mashakani

Katika hatua nyingine, Kamishna Mkuu wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa Michelle Bachelet ameelezea hofu yake kubwa juu ya maelfu ya raia walionasa katikati ya maeneo ya mapigano kwenye mji mkuu wa Libya, Tripoli na viunga vyake.

Akizungumza mjini Geneva, Uswisi hii leo, Bi. Bachelet amesisitiza umuhimu wa kutenga haraka maeneo salama kwa raia hao kupenya na kuweza kuondoka huku akitoa wito pia wa sitisho la mapigano na kuanza tena kwa mazungumzo baina ya pande kinzani.

Maeneo yaliyoathirika zaidi ni viunga vya Tripoli ambavyo ni Aziziya, Swani na Ain Zara ambapo ongezeko la  mashambulizi kutoka angani yanayoambatana na makombora mazito kwenye maeneo ya raia yanazidi kuathiri wananchi wasio na hatia sambamba na kuharibu miundombinu.

“Mwendelezo wa mashambulizi kwenye makazi ya raia, ikiwemo kutumia maroketi na kuangusha makombora kutoka angani kunatia zaidi wasiwasi. Maisha ya maelfu ya watoto, wanawake na wanaume yako mashakani. Ingawa takwimu zinaonyesha kuwa raia waliouawa ni 22 na majeruhi 74, namba halisi zinaweza kuwa juu zaidi,” amesema Bi. Bachelet.

Amekumbusha pande zote kwenye mzozo wa Libya ya kwamba matumizi ya silaha zinazolipuka kwenye maeneo ya raia bila uangalifu wowote ni ukiukwaji wa haki za kibinadamu za kimataifa na haki za usaidizi wa kibinadamu.

Michelle Bachelet, Kamishna Mkuu wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa.
UN Photo - Jean-Marc Ferre
Michelle Bachelet, Kamishna Mkuu wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa.

Usalama wahamiaji walio korokoroni

Kamishna Mkuu huyo wa haki za binadamu pia ameelezea wasiwasi wake kuhusu hatma ya wahamiaji na wakimbizi 3,350 akihofu kuwa usalama wao uko mashakani wakati huu ambapo bado wanashikiliwa kwenye rumande zilizoko maeneo ya mapigano.

Ofisi ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa inasema takribani wahamiaji 12 walijeruhiwa na wapiganaji tarehe 23 mwezi hu u karibu na eneo la Qasr ben Gasheer, kabla ya kuhamishiwa kituo kingine.

Halikadhalika vituo hivyo ambamo kwavyo wahamiaji na wakimbizi hao wanashikiliwa vinakabiliwa na uhaba mkubwa wa chakula na maji na kwamba baadhi ya walinzi wametelekeza vituo hivyo na hivyo kuweka usalama wa wahamiaji hao mashakani.

“Wahamiaji wanapaswa kuhamishwa kutoka vituo hivyo korokoroni haraka iwezekanavyo na badala yale wapate huduma za ulinzi za kibinadamu ikiwemo kupata makazi na maeneo mengine ambayo ni salama,” amesema Bi. Bachelet.

 

♦ Kupata takwimu za waathirika vitani Ukraine bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter