Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hali ya mambo bado ni tete mjini Tripoli Libya:UN

Wahamiaji kutoka kituo walimokuwa wakishikiliwa nchini Libya na kusafirishwa hadi Niger
UNHCR/Jehad Nga
Wahamiaji kutoka kituo walimokuwa wakishikiliwa nchini Libya na kusafirishwa hadi Niger

Hali ya mambo bado ni tete mjini Tripoli Libya:UN

Amani na Usalama

Yumkini hali ya mambo bado si shwari kwenye mji mkuu wa Libya, Tripoli ambako tangu kuzuka machafuko wiki iliyopita takriban raia 21 wameuawa wakiwemo wanawake na watoto huku 16 wakijeruhiwa. Sasa Umoja wa Mataifa watoa wito kwa pande kinzani kuwanusuru raia hao.

Kwa mujibu wa mpango wa Umoja wa Mataifa nchini Libya UNSMIL, wahudumu wa misaada walipigwa risasi Jumamosi Septemba Mosi wakijaribu kuwaokoa raia waliokwama karibu na eneo la Khilat al-Firjan .

Pande kinzani katika mzozo huo zimekuwa zikivurumisha makombora kwenye maeneo yaliyo na watu wengi ikiwemo kutumia maroketi, magruneti, vifaru na silaha zingine nzitonzito, huku kundi lenye silaha la al-Kaniyat likishutumiwa kupora magari matatu ya kubebea wagonjwa kutoa idara ya dharura na huduma za magari ya wagonjwa.

Sasa ofisi ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa imetoa wito kwa pande zote kukomesha mashambulizi hayo na kuchukua kila tahadhari kuwalinda raia na mali zao. Liz Throssell ni msemaji wa ofisi ya haki za binadamu mjini Geneva Uswis.

(SAUTI YA LIZ THROSSELL)

OHCHR pia inahofia athari za vita hivyo kwa makundi yasiyojiweza na yaliyo katika hali tete wakiwemo wahamiaji na wakimbizi wa ndani. Karibu wahamiaji 8,000 walioko kwenye mahabusu wamekwama kwenye vituo hivyo katika maeneo ambako mapigano yanafanyika, bila kuwa na fursa ya kupata chakula au huduma za matibabu. Wengine wameachiliwa lakini hawajaweza kupata usalama na huduma muhimu , wakati wahamiaji wengine katika mahabusu wamearifiwa kutekwa na makundi yenye silaha na kuwashinikiza kuwafanyia kazi.”

Mwanamke kutoka Tawargha akiwa mbele ya banda lake katika hifadhi ya wakimbizi katika mji wa Tripoli
UNHCR/Tarik Argaz
Mwanamke kutoka Tawargha akiwa mbele ya banda lake katika hifadhi ya wakimbizi katika mji wa Tripoli

Nayo mashirika ya misaada ya kibinadamu yanasema hali ya kibinadamu inazidi kuzorota, na kufanya kuwa mtihani kuwafikia wanaohitaji msaada muhimu. Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR Jumatatu lilifanikiwa kuzitembelea familia zilizoathitika na kutathimini hali yao kwa ushirikiano na mashirika mengine ya misaada. UNHCR itatoa msaada wa dharura kwa watu wote 150 wanaopata hifadhi katika shule moja. Charlie Yaxley ni msemaji wa UNHCR ameongeza kuwa

(SAUTI YA CHARLIE YAXLEY)

“Hali hivi sasa kwenye mji mkuu wa Libya ni tete, isiyotabirika na inazuia fursa kwa mashirika ya misaada ya kibinadamu kuwafikia wakimbizi wa ndani ambao ni Walibya, na wakimbizi wengine walioathirika na machafuko.”

UNHCR imesema inaendelea kufuatilia kwa karibu hali mjini Tripoli kwa kushirikiana na kituo cha Libya cha kukabiliana na wahamiaji haramu na mashirika mengine ya misaada ya Umoja wa Mataifa na kuchagiza kuwa, wakimbizi wote na wahamiaji wahamishiwe katika maeneo yenye usalama.

TAGS: Libya, Tripoli, Machafuko, UNHCR, ofisi ya haki za binadamu.