Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hali inaendelea kuwa tete Libya-OCHA

Miaka 8 tangu kuondolewa kwa utawala wa Ghadaffi nchini Libya, bado nji ya kuelekea katika amani na usalama imesalia kizungumkuti.
OCHA/Giles Clarke
Miaka 8 tangu kuondolewa kwa utawala wa Ghadaffi nchini Libya, bado nji ya kuelekea katika amani na usalama imesalia kizungumkuti.

Hali inaendelea kuwa tete Libya-OCHA

Amani na Usalama

Ripoti kutoka ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kuratibu misaada ya dharura, OCHA, iliyochapishwa hii leo inasema mapigano ya kutumia silaha nzito na mashambulizi kutoka angani vimeendelea katika maeneo kadhaa ya mji mkuu wa Libya, Tripoli na viungani.

Ripoti inanukuu vyanzo vya kuaminika ambavyo havijathibitishwa, vikisema kuwa  usiku wa kuamkia leo, katika viunga vya Tripoli, miongoni mwa mengine yakiwemo maeneo ya Abusliem, Souq Jumaa na Hadbaa, makombora yamesababisha vifo vya watu sita wakiwemo wanawake wanne na kuwajeruhi watu wengine 20.

OCHA inasema tangu kuanza kwa vurugu, inakadiriwa kuwa watu 80 wamejeruhiwa na wengine 20 wamepoteza maisha lakini wale ambao wamethibitishwa ni wananchi 54 kujeruhiwa na wengine 14 kupoteza maisha.  

Ripoti ya sasa imeonesha ongezeko la wanaokosa makazi kwa siku, ambapo zaidi ya watu 4,500 ni watu wapya waliopoteza makazi kiasi kinachoongeza idadi ya wakimbizi wa ndani kufikia 25,000. Wananchi wengi waliokwama katika maeneo yenye mgogoro wamejikuta katika sintofahamu ya kutokujua ikiwa wabaki katika majumba yao au waondoke kwa sababu ya hali mbaya iliyoko huko nje ya mapigano na mabomu. Hali hiyo ya sintofahamu inazidi kuongezeka kwani chakula na mahitaji mengine muhimu vinazidi kupungua.

Mgogoro wa sasa umeongeza hatari zaidi kwa watu baada ya mgogoro wa miaka mingi, mgogoro wa kiuchumi na kijamii na upungufu katika huduma za kijamii ambazo tayari zimewaweka takribani watu 820,000 waakiwemo watoto 250,000 katika uhitaji mkubwa wa misaada ya kibinadamu.

Kutokana na hali inayoendelea usiku wa kuamkia leo, mwakilishi maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini Libya Ghassan Salamé ambaye pia ni mkuu wa ujumbe wa Umoja wa Mataifa  nchini Libya, UNSMIL, kupitia ukurasa wake wa twitter ameeleza wasiwasi alionao juu ya mstakabali wa wakazi wa Tripoli, akisema “usiku wa kutisha wa makombora katika wa maeneo ya makazi. Kwa ajili ya raia milioni 3 wanaoishi katika Greater Tripoli, mashambulizi haya yanapaswa kukoma. SASA!”