Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Machafuko mapya Tripoli yawafungisha virago zaidi ya watu 2800: Ribeiro

Watu walioshikiliwa kwenye mji mkuu wa Libya, Tripoli, wakisubiri kuhamishiwa eneo salama. Pichani Msichana kutoka Eritrea mwenye umri wa miaka 19 akizungumza na mfanyakazi wa UNOCHA akisubiri kupanda basi kuelekea kituo cha mpito kabla ya kwenda Niger.
UN OCHA/GILES CLARKE
Watu walioshikiliwa kwenye mji mkuu wa Libya, Tripoli, wakisubiri kuhamishiwa eneo salama. Pichani Msichana kutoka Eritrea mwenye umri wa miaka 19 akizungumza na mfanyakazi wa UNOCHA akisubiri kupanda basi kuelekea kituo cha mpito kabla ya kwenda Niger.

Machafuko mapya Tripoli yawafungisha virago zaidi ya watu 2800: Ribeiro

Wahamiaji na Wakimbizi

Machafuko yanayoendelea ndani ya mji mkuu wa Libya Tripoli na viunga vyake yamesababisha zaidi ya watu 2800 kufungasha virago wakikimbia mapigano, pia yamezuia huduma za dharura kuwafikia majeruhi na raia, na kuharibu mfumo wa umeme.

Hayo ni kwa mujibu wa mratibu wa masuala ya kibinadamu wa Umoja wa Mataifa nchini Libya, Maria Ribeiro akiongeza kwamba hali ya kibinadamu na ulinzi wa raia viko mashakakani na kwamba wimbi hili la machafuko limezidisha zahma kwa wakimbizi na wahamiaji ambao wanashikiliwa kwenye vituo ambako mapigano yanaendelea.

Bi. Ribeiro, amezikumbusha pande zote kinzani katika mzozo nchini Libya kwamba zina wajibu chini ya sheria za kimataifa za binadamu na haki za binadamu wa kuhakikisha usalama wa raia wote, miundombinu yao ikiwemo shule, hospitali na mifumo ya huduma za umma na pia kuruhusu bila vikwazo wala masharti yoyote misaada ya kibinadamu kuwafikia wanaoihitaji katika maeneo yaliyoathirika na machafuko.

Mratibu huyo amesema Umoja wa Mataifa unaendelea kutoa wito wa kuwepo makubaliano ya muda ya amani ili kuruhusu masuala ya kibinadamu kufanyika ikiwemo kutoa huduma za dharura na kuruhusu raia kuondoka kwa hiyari kwenye maeneo yenye mapigano wakiwemo majeruhi.

Jumuiya ya kimataifa ya masuala ya kibinadamu inafuatilia kwa karibu hali inayoendelea Libya na tayari imeshajiandaa kwa huduma za dharura za kibinadamu kwa ajili ya kuwasaidia raia ambako kutahitajika.

Mwanamke akilia baada ya kuokolewa baharini nchini Libya
UNHCR/Hereward Holland
Mwanamke akilia baada ya kuokolewa baharini nchini Libya

Mashirika mengine

Wakati huohuo shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi , UNHCR limesema linahofia maisha ya nmaelfu yawakimbizi na wahamiaji wanaoshikiliwa katika vituo mbalimbali nchini Libya.

Hivi sasa shirika hilo limetayarisha misaada kwa ajili ya familia 500 Kusini mwa Tripoli na Misrata kwa ajili ya mahitaji ya wakimbizi wa ndani. UNHCR inaratibu misaada hiyo kupitia mshirika wake LibAis na wahudumu wengine wa dharura.

Ikishirikiana na wadau wengine UNHCR inafanya kila liwezekanalo ili kuhakikisha usalama wa wakimbizi na wahamiaji walioko kwenye vituo mahali ambako vita vinaendelea ikiwa ni pamoja na kujadiliana na serikali ili kuruhusu watu hao kuhamishwa na kupelekwa kwenye kituo kipya cha GDF. Kwa muda wa wiki mbili zilizopita UNHCR imeongeza kasi ya uandikishaji wa wakimbizi wanaoishi maeneo ya mijini  na tangu kuanza mwaka huu 2019 , UNHCR imeshaorodhesha wakimbizi 2,426

Hatua zilizofanyika hadi sasa

Hadi kufikia sasa wakimbizi wa ndani wamesajliwa ambapo 2,800 kati yao wanasemekana kutawanywa na machafuko haya mapya ya mjini Tripoli. Asilimia kubwa ya wakimbizi hao wa ndani wamehamia kwa ndugu na jamaa na wengine wanapatiwa hifadhi katika malazi ya Tajoura.

Halikadhalika hadi jana  Aprili 7 wakimbizi na wahamiaji 996 wameokolewa baharini japo idadi ya wakimbizi na wahamiaji wanaoingia Libya imepungua kwa kiasi kikubwa kuanzia Januari.

Kwa mujibu wa UNHCR kwa mwaka huu idani kubwa ya wakimbizi na wahamiaji wanaoingia Libya wanatokea Core D’voire, Sudan, Mali, na Somalia.