Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ni sawa kuzipatia nchi misaada ya maendeleo lakini pia tuzijengee uwezo zijikwamue- Guterres

Miradi ya FAO ya kuwawezesha wakulima kama hawa kupata stadi za kilimo bora, inaongeza uzalishaji na  hivyo kuinua kipato cha wakulima.
UNDP Uganda/Luke McPake
Miradi ya FAO ya kuwawezesha wakulima kama hawa kupata stadi za kilimo bora, inaongeza uzalishaji na hivyo kuinua kipato cha wakulima.

Ni sawa kuzipatia nchi misaada ya maendeleo lakini pia tuzijengee uwezo zijikwamue- Guterres

Ukuaji wa Kiuchumi

Mkutano wa Nne wa uchangishaji fedha kwa ajili ya maendeleo, FfD umeanza leo kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa jijini New York, Marekani ambapo Katibu Mkuu António Guterres amesema, “tunahitaji fedha zaidi ili kutekeleza na kufanikisha malengo ya maendeleo endelevu, SDGs.”

Akihutubia washiriki wakiwemo mawaziri kutoka mataifa yapatayo 30, Bwana Guterres amesema kila mtu anapaswa kufikia malengo hayo akisema hususan nchi  zilizoendelea zinapaswa kutimiza ahadi zao za kuchangia fedha kwa ajili ya maendeleo.

Katibu Mkuu amesema kuna mbinu za kutokomeza umaskini, ukosefu wa usawa, mabadiliko ya tabianchi na changamoto za mazingira akisema mbinu hizo ni SDGs, zilizopitishwa 2015, ajenda ya utekelezaji ya Addis Ababa na mkataba wa Paris wa mabadiliko ya tabianchi.

Utafiti wa hivi karibuni wa shirika la fedha duniani, IMF ulibaini kuwa nchi zinazoendelea zinakabiliwa na wastani wa pengo la fedha takribani dola trilioni 2 kwa mwaka kwa ajili  ya uwekezaji kwenye sekta za afya, elimu, barabara, umeme, maji na huduma za kujisafi.

Inaelezwa kuwa “kwa nchi zinazoendelea, hii inamaanisha nyongeza ya matumizi ya takribani asilimia 15 ya pato la ndani la taifa kila mwaka.” Imesema IMF.

Bwana Guterres amesema, “msaada wa maendeleo unasalia kuwa muhimu, hususan kwa nchi maskini zaidi lakini katu tusisahau kusaidia uwezeshaji wa nchi hizo kuweza kujipatia wenyewe mapato na ndani.”

Katibu Mkuu amesema, “hii inamaana kupata mapato kutokana na kodi. Hii pia inahitaji jamii ya kimataifa kuchukua hatua zaidi kutokomeza ukwepaji wa kodi, utakatishaji wa fedha na usafirishaji wa fedha  nje ya nchi ambao unakwamisha juhudu za kupata fedha za uwekezaji.”

Harakati za kilimo na ufugaji zikiendelea barani Afrika.
©FAO/Gustave Ntaraka
Harakati za kilimo na ufugaji zikiendelea barani Afrika.

Kwa mujibu wa Guterres, hatua hizo pekee iwapo zitafanikiwa, zinaweza kutosheleza kufadhili huduma za umma ambazo ni muhimu katika kufanikisha SDGs, hasa kwenye nchi zinazoibuka kiuchumi.

Amegusia pia mifumo ya sera akisema nayo pia ni muhimu katika kupunguza hatari na zinaweza mazingira bora ya biashara, kuhamasisha uwekezaji kwenye sekta ya umma na kuoanisha mifumo ya fedha na malengo ya maendeleo endelevu kwa muda mrefu.

Amesisitiza kuwa, “ lazima tuongeze fursa ya watu kupata fedha ambazo zitasaidia wanawake na wafanyabiashara wadogo na wakati. Teknolojia mpya za mifumo ya fedha, taasisi na masoko ni muhimu katika kupanua wigo wa mfumo jumuishi wa fedha na kufanikisha uwekezaji.”

Kwa upande wake, Naibu Mkurugenzi mwendeshaji wa shirika la fedha duniani, IMF, Tao Zhang, amesema, “ hakuna jambo linaleta mvutano kama biashara. Lazima tushirikiane ili kutatua mivutano ya kibiashara na kupanga upya mfumo wa biashara ya kimataifa.”

Malengo ya maendeleo endelevu, SDGs  yako 17.
UN SDGs
Malengo ya maendeleo endelevu, SDGs yako 17.

Ameongeza kuwa biashara ya bidhaa, huduma na uwekezaji ambavyo ni huru, na haki na yenye maslahi kwa kila mtu ni injini ya msingi kwa ajili ya ukuaji uchumi na kuweka fursa za ajira.

Akizungumza naye kwenye mkutano huo, afisa mwandamizi kutoka Benki ya Dunia, Mahmoud Mohieldin, amesema kuendelea kufanya biashara kama kawaida hakutowezesha nchi kutokomeza umaskini uliokithiri ifikapo mwaka 2030.

Mkutano huo wa nne wa uchangishaji fedha kwa ajili ya maendeleo ambao unasimamiwa na Baraza la Uchumi na Kijamii la Umoja wa Mataifa, ECOSOC, unatathmini ajenda ya  utekelezaji ya Addis Ababa au Ajenda ya Addis, na makubaliano mengine ya kufanikisha SDGs na utamalizika tarehe 18 mwezi huu wa Aprili.