UNMISS yasaidia Upper Nile kuchukua hatua kusongesha amani

12 Aprili 2019

Nchini Sudan Kusini kwenye jimbo la Upper Nile, mkutano ulioitishwa na ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini humo kwa lengo la kurahisisha utekelezaji wa mkataba mpya wa amani umezaa matunda na hivyo kuleta nuru katika utokomezaji wa ukatili wa kingono na usambazaji misaada ya kibinadamu.
 

Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Sudan Kusini, UNMISS ulichukua hatua ya kuleta pamoja magavana wa jimbo la Upper Nile na makamanda waandamizi kwa lengo la kuona jinsi gani ya kutekeleza mkataba huo mpya wa amani wa mwaka 2018 kwenye jimbo hilo.

Mkutano  huo wa siku tatu ukiwa wa kwanza kuleta wajumbe wengi wa upande wa upinzani ulifanyika mjini Malakal ukishamirishwa na nyimbo zilizoimbwa na washiriki ili kujenga mshikamano.
Viongozi walijadili kwa kina suala la wahudumu wa kibinadamu pamoja na kuondoa vikundi vilivyojihami ambavyo vinakwamisha usambazaji huduma.

Kamanda wa kikosi huko Malakal Meja Jenerali Akol Ajok anasema,  “tumeazimia amani kwasababu amani ni ya kila mt una tuna dhma ya kutekeleza kupata amani. Ingawa amani ni ya kila mtu mipango ya usalama ni muhimu ili hatimaye serikali iwe na amani na mfumo wa serikali uweze kwenda sambamba na mkataba mpya wa amani.”

Mwishoni mwa mkutano huo katika uwanja wa mpira wa Malakal, pande zote zilizitia saini ahadi ya maandishi ikiwemo  kutokomeza ukatili wa kingono na wa kijinsia, kuondoa vizuizi kwa watoa huduma, kuachilia huru wafungwa, kusitisha harakati za vikundi binafsi vilivyojihami.

Hazel de Wet ni Mkuu wa ofisi ya UNMISS jimboni Upper Nile ambaye anasema kwamba , “wameweka ahadi thabiti kuelekea amani, uhuru wa kutembea, kuendeleza na kusongesha haki za binadamu na wako makni kuhakikisha wakimbizi wa ndani na wakimbizi wanarejea salama makwao na kwa utu. Na hizi ni ahadi muhimu zilizopitishwa na serikali na upinzani pamoja na makamanda wa kijeshi.”
 

 

♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter