Sudan Kusini hawaombi mambo mengi isipokuwa usalama wa familia zao-Balozi Craft

23 Oktoba 2019

Mwakilishi wa kudumu wa Marekani katika Umoja wa Mataifa Balozi Kelly Craft amezuru mji wa Malakal nchini Sudan Kusini ambako amekutana na wanawake kutoka katika maeneo  ya ulinzi wa raia na pia akatembelea kituo cha kuzalisha maji cha shirika la World Vision ambacho kinasaidia kupunguza uhaba wa maji safi na ya kunywa.

Miaka mitano iliyopita, mji wa Malakal ulisambaratishwa na vurugu kati ya vikosi vya serikali na vile vya upinzani ambapo watu wengi walichinjwa mitaani na kulazimishwa kuyakimbia makazi yao na kutafuta hifadhi katika kambi ya mpango wa Umoja wa Mataifa nchini Sudan Kusini UNMISS.

Hivi leo mji umejawa na shughuli. Ingawa watu 32,000 waliotawanywa bado wanaishi katika maeneo ya ulinzi wa raia, hivi sasa wanatembea kwa uhuru kati ya kambi na mji na usalama unaboreshwa kutokana na makubaliano ya amani na kusitisha mapigano.

Ziara ya Balozi Craft inafuatia mlolongo wa mikutano ya ngazi ya juu kati ya wajumbe wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na viongozi wa kisiasa wa Sudan akiwemo Rais Salva Kiir na kiongozi wa upinzani Dkt Riek Machar. Balozi Craft anasema,“kila mtu hapa ana matumaini na hawaombi mengi isipokuwa usalama kwa familia zao, kuweza kuzihudumia familia zao, na wana imani hiyo. Nataka pia kuzungumzia kuhusu Umoja wa Mataifa na ilivyo muhimu kwamba wamekuwa hapa. Ni msaada kwa watu wengi hapa na nadhani ni muhimu zaidi kwamba Serikali ione hivyo na ichukue jukumu pia na kufanya mabadiliko yasiyo na vizingiti "

Wakati wa ziara yake hiyo akiwa na wajumbe wenzake wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, ameshiriki doria katika mto Nile akiwa na kikosi cha UNMISS na wote kwa pamoja wakaahidi kuiunga mkono Sudan Kusini katika mchakato wa amani.

 

 

♦ Kutembelea ukurasa maalum wa UNGA76 bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter