Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kiu ya amani Sudan Kusini ni dhahiri- Shearer

Katika picha hii kutoka maktaba, Ronda, (kulia) mmoja wa wakimbizi wa ndani akifua nguo zake kwenye kituo cha kufadhi raia huko Wau Sudan Kusini.
UNICEF/Ohanesian (maktaba)
Katika picha hii kutoka maktaba, Ronda, (kulia) mmoja wa wakimbizi wa ndani akifua nguo zake kwenye kituo cha kufadhi raia huko Wau Sudan Kusini.

Kiu ya amani Sudan Kusini ni dhahiri- Shearer

Amani na Usalama

Mwakilishi maalumu wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini Sudan kusini, David Shearer, ametembelea eneo la Bahr El Ghazal nchini humo ambako amekuwa na mazungumzo na viongozi kuhusu masuala mbalimbali ikiwemo utekelezaji wa mkataba wa amani, kusaidia wakimbizi wa ndani kurejea kwa hiyari katika maeneo yao na pia kuhusu suala la usalama katika ukanda huo.

Katika ziara hiyo Shearer ambaye pia ni mkuu wa ujumbe wa  Umoja wa Mataifa nchini Sudan Kusini, UNMISS, likutana na Jenerali Jal Malith Jal Gavana wa Aweil kujadili masuala kadhaa kuhusu utekelezaji wa mkataba wa amani uliotiwa saini mwezi Septemba 2018. Na baada ya kutoka katika ofisi ya Gavana wa Aweil akafanya mkutano na Gavana wa Aweil Mashariki, Deng Deng Akuei katika mkutano uliofanyika katika kambi ya Umoja wa Mataifa mjini Aweil.

Baada ya mkutano huo David Shearer akaeleza kuwa amefurahishwa na hali ya Aweil ambayo imesalia na utulivu kwa muda sasa kwa kuwa, “viongozi katika maeneo yote mawili ya Aweil na Aweil Mashariki wako mstari wa mbele hawana shida na mgogoro. Kumetulia kwa hivyo wanaangalia hatua inayofuata. Wanataka kuyaendeleza maeneo yao, wanataka kurekebisha, wanataka kuwa na fedha za maendeleo na kuwekeza. Kama itatokea hivyo, dalili zipo kwamba Aweil itanyanyuka.”

Baada ya mkutano huo akaelekea katika mji wa Wau ambao ni wa  pili kwa ukubwa nchini Sudan Kusini, ambako alikutana na viongozi kutoka upande wa serikali na wa upinzani.

Hapa akasihi kuwe na suluhu katika mgogoro kati ya wafugaji na wakulima, mgogoro ambao umesababisha vifo kwa watu kadhaa katika wiki za hivi karibuni.

Gavana wa Wau Angelo Taban Biajo akaeleza hatua ambazo amepiga katika eneo lake ili kuleta amani akisema kuwa, “tumeifunika eneo lote la usalama kwa asilimia 99.9 na suala jingine ambalo linabaki ni kuwahamisha watu wetu kurejea katika  maeneo yao ya makazi na mashamba yao ili waweze kuendeleza maisha yao kawaida kama hapo awali. "

Kama ilivyo kwa gavana, wananchi wengi wanasubiri utekelezwaji kamili wa mkataba wa amani ili kuweka njia ya kurejea katika maisha ya kawaida.