Kampeni ya usafi Wau yahamasisha wakimbizi kurejea nyumbani:UNMISS 

13 Februari 2019

Kampeni kubwa inafanyika jimboni Wau nchini Sudan Kusini  kwa ushirikiano wa Umoja wa Mataifa, serikali na wenyeji ili kujenga mazingira salama na stahiki na hatimaye familia za wakimbizi wa ndani zilizotawanywa na miaka ya vita vya wenyewe kwa wenyewe ziweze kurejea nyumbani. 

Ni katika mitaa ya Aweil Gadidi mjini Wau, wanawake kwa wanauume wakiwemo pia walinda amani wa mpango wa Umoja wa Mataifa Sudan Kusini UNMISS wako katika harakati za kusafisha na kukusanya taka akiwemo mkazi wa Wau Regina Fidele anayeamini kuwa nyumbani ni nyumbani hata iweje.

“Ninafanya kazi Kur Lulu na Shuk Jou, nimekuja hapa kusafisha. Meya ametoa wito kwa watu kuja kusaidia kazi ya usafi Awiel Gedid”

Eneo hili awali watu wake walijivunia sana lakini baada ya vita kuzuka maelfu ya familia zilifungasha virago kusaka usalama wengine katika kambi ya ulinzi wa raia ya Umoja wa Mataifa ya Wau. Na baada ya makubaliano ya amani Septemba mwaka jana matumaini ya kurejea nyumbani yakaanza kufufuka lakini mji hautamaniki kwa kuwa ulitelekezwa ndipo UNMISS ikachukua usukani wa kampeni ya usafi ukishirikisha wadau wote wakiwemo wenyeji wa Wau .

Mbali ya usafi kampeni hiyo inataka kuhakikisha watu wanaorejea wanajihisi salama . Sam Muhumure ni mkuu wa UNMISS wa ofisi za mashinani

“Tutalifanyia kazi suala la usalama kwa kushirikiana na serikali kama ambavyo tumekuwa tukifanya , kuimarisha doria katika maeneo hayo,kubaini baadhi ya changamoto za usalama zinazojitokeza na kuhakikisha kwamba kwa pamoja tunaweka mfumo kwa kuzishughulikia mara moja. Sasa zaidi ya hilo watu pia wanahitaji msaada wa chakula , wanahitaji msaada wa malazi.”

Kwa mujibu wa chifu wa eneo hilo la Angelo Ding kampeni hii imewahamasisha wengi kurejea nyumbani kwa hiyari na mpaka sasa takribani watu 500 wamesharejea.

 

 

♦ Kutembelea ukurasa maalum wa UNGA76 bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter