Huduma ya afya kwa wote ni haki si upendeleo- WHO

7 Aprili 2019

Leo ni siku ya afya duniani ambapo Umoja wa Mataifa unapatia mkazo suala la huduma ya afya kwa wote.

Mkurugenzi Mkuu wa shirika la afya ulimwenguni, WHO Dkt. Tedros Ghebreyesus amesema suala la huduma ya afya kwa wote ni lengo kuu la shirika hilo akisema hatua muhimu ya kufanikisha ni kuhakikisha kila mtu anapata huduma anayohitaji, pindi anapohitaji pale pale kwenye jamii yake.

Akizungumza mjini Geneva, Uswisi, Dkt. Ghebreyesus amesema ingawa kuna maendeleo yamefikiwa katika baadhi ya nchi za maeneo mbalimbali dunia kuona kila mtu anapata huduma ya afya, bado mamilioni ya watu wanalazimika kuchagua kati ya huduma ya afya na mlo, mavazi au hata makazi.

 “Tupo hapa kuweka kauli thabiti kuwa afya ni haki na si upendeleo. Tupo hapa kusema kuwa watu wote wana haki ya kupata huduma ya afya wanayohitaji, pindi wanapotahiaji  bila mkwamo wowote wa kifedha,” amesema Mkurugenzi Mkuu  huyo wa WHO wakati wa tukio maalum lililofanyika mjini Geneva.

Mhudumu  wa afya akitoa huduma kwa mkimbizi mjamzito katika kituo cha afya katika kambi ya wamkimbizi Nayapara
UNFPA Bangladesh/Allison Joyce
Mhudumu wa afya akitoa huduma kwa mkimbizi mjamzito katika kituo cha afya katika kambi ya wamkimbizi Nayapara

Amesema WHO ndio mwamba wa huduma ya afya ya msingi kwa wote na kwamba, “huduma ya afya ya msingi kwa wote inahusisha mahitaji yote makubwa ya afya ya binadamu. Inasaidia pia kuepusha watu kwenda hospitali na kusalia kwenye jamii zao.”

Kwa mantiki hiyo amesema katika siku ya afya duniani mwaka huu wa 2019, wanatoa wito kwa mataifa kuwekeza katika huduma za msingi za afya.

Amekumbusha kuwa maadhimisho ya mwaka huu ya siku ya afya duniani, yanafanyika katikati ya mkutano wa afya kwa wote uliofanyika Astana, Kazakhstan mwezi Oktoba mwaka jana na kikao cha ngazi ya juu kuhusu afya kwa wote kitakachofanyika wakati wa mkutano wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mjini New York, Marekani  mwezi Septemba mwaka huu wa 2019.

Mambo Muhimu kuhusu huduma ya afya kwa wote

  • Takribani nusu ya wakazi wa dunia bado hawapati huduma za msingi za afya.
  • Takribani watu milioni 100 bado wanasukumwa kwenye ufukara kwa kuwa hawana uwezo wa kulipia huduma zao za afya.
  • Zaidi ya watu milioni 800 , sawa na asilimia 12 ya wakazi wote wa dunia, wanatumia asilimia 10  ya kipato cha kaya kugharimia huduma za afya.
  • Mataifa  yote 193 wanachama wa Umoja wa Mataifa wamekubaliana kufikia lengo la huduma ya afya kwa wote ifikapo mwaka 2030, ikiwa ni sehemu ya malengo ya maendeleo endelevu, SDGs.

 

 

♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter