Si haki mtu kupaswa kuchagua kati ya kununua dawa au chakula- Espinosa
Si haki mtu kupaswa kuchagua kati ya kununua dawa au chakula- Espinosa
Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa leo limekuwa na mjadala ulioleta pamoja wadau mbalimbali kujadili kuhusu huduma ya afya kwa wote duniani ikiwa ni maandalizi ya mkutano wa ngazi ya juu wa viongozi wa nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa kuhusu mada hiyo mwezi Septemba mwaka huu.
Tukio hilo lililofanyika kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa jijini New York, Marekani lilikuwa na vikao vitatu vikijadili mada kuu tatu ambazo zilitoa fursa kwa wadau wakiwemo wawakilishi wa serikali na mashirika ya kiraia kuchangia hoja.
Mada hizo ni huduma ya afya kwa wote kama kichochea cha maendeleo shirikishi na ustawi, afya kwa wote kama ahadi ya kuleta uwiano na dhima ya wadau mtambuka kwenye suala la huduma ya afya kwa wote na uwekezaji.
Akifungua mkutano huo, Rais wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa Maria Fernanda Espinosa amesema, “ni ajabu kuwa miongo saba tangu afya itambuliwe kuwa ni haki ya msingi ya binadamu kwenye tamko la haki za binadamu la Umoja wa Mataifa mwaka 1948, bado huduma afya imesalia ndoto kwa mamilioni ya watu waonahaha kupata huduma hiyo.”
Bi. Espinosa amesema takribani “nusu ya idadi ya watu duniani hawana uwezo wa kufikia huduma za msingi za afya. Kila mwaka gharama ya huduma ya afya inasukuma zaidi ya watu milioni 100 kwenye lindi la umaskini.”
Amesema watu hao wanashinikizwa kufanya uchaguzi wa mambo ambayo hakuna mtu anapaswa kuchagua kati ya kununua dawa au chakula.
Benki ya Dunia inakadiria kuwa ili kufanikisha malengo ya maendeleo endelevu, SDGs, kuhusu maji na huduma za kujisafi kwa wote, ulimwengu unahitaji dola bilioni 114 kila mwaka.
Mkutano huo pia ulihutubia na Mkurugenzi Mkuu wa shirika la afya ulimwenguni, WHO, Dkt. Tedros Ghebreyesus, ambaye aliwasilisha hotuba yake kwa njia ya video kutoka Goma jimbo la Kivu Kaskazini nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC aliko ziarani.
Dkt. Tedros amesisitiza kuwa huduma ya afya ya msingi ni jawabu muafaka hata katika kuhakikisha kuwa ugonjwa wa Ebola unatokomezwa.
“Huduma ya afya ya msingi ni mwamba wa huduma ya afya kwa wote. Inaweza kusaidia kuzuia au kupunguza madhara ya milipuko na dharura nyingine za magonjwa kama Ebola. Utayari, kinga na uendeleza wa huduma za afya unaweza kushamiri,” amesema Dkt.Tedros huku akipongeza mataifa ambayo tayari yako kwenye mwelekeo wa kufanikisha huduma ya afya kwa wote.
Ametaka nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa kutumia fursa ya mkutano wa mwezi Septemba kuhakikisha lengo hilo la huduma ya afya kwa wote linafikiwa mwaka 2030.