Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

WHO na FACEBOOK waungana kukabili habari potofu kuhusu chanjo

Shirika la afya ulimwenguni, WHO linashirikiana na Facebook kukabiliana na kuenea kwa taarifa potofu kuhusu chanjo katika mitandao ya kijamii (Septemba 2019)
UN Photo/Manuel Elías
Shirika la afya ulimwenguni, WHO linashirikiana na Facebook kukabiliana na kuenea kwa taarifa potofu kuhusu chanjo katika mitandao ya kijamii (Septemba 2019)

WHO na FACEBOOK waungana kukabili habari potofu kuhusu chanjo

Afya

Shirika la afya ulimwenguni, WHO limeingia ubia na kampuni ya Facebook ili kusaidia kusambaza taarifa sahihi kuhusu chanjo.

Mkurugenzi Mkuu wa WHO Dkt. Tedros Ghebreyesus amekaribisha kwa moyo wa dhati ubia huo ambao kwao, kampuni hiyo ya Facebook itahakikisha watumiaji wake pindi wanasaka taarifa na ushauri kwenye majukwaa yake kama vile Instagram, Facebook, makundi, kurasa na majukwaa wanapata taarifa sahihi.

Kwa mantiki hiyo, Facebook itaelekeza mamilioni ya watumiaji wake kwenye taarifa sahihi za WHO kuhusu chanjo kwa kutumia lugha mbalimbali ili kuhakikisha ujumbe muhimu kuhusu afya unafikia wale wanaohitaji zaidi.

Kwa miezi kadhaa WHO na Facebook wamekuwa kwenye majadiliano kuhakikisha kuwa watumiaji wa mitandao hiyo wanapata taarifa sahihi kuhusu chanjo na hivyo kupunguza kuenea kwa taarifa potofu.

Dkt. Tedros anasema taarifa potofu kuhusu chanjo ni tishio kubwa kwa afya duniani na zinaweza kutokomeza maendeleo yaliyopatikana katika kukabiliana na magonjwa yanayozuilika.

Mshauri wa mashinani kutoka UNICEF huko jimboni Kayes nchini Mali  akimweleza mama umuhimu wa kumpatia chanjo mwanae. (Machi 2019)
UNICEF/Seyba Keïta
Mshauri wa mashinani kutoka UNICEF huko jimboni Kayes nchini Mali akimweleza mama umuhimu wa kumpatia chanjo mwanae. (Machi 2019)

Hata hivyo Dkt. Tedros amesema juhudi hizi za mtandaoni zinapaswa kwenda sambamba na hatua thabiti za serikali na sekta ya afya za kuendelea kujenga iamni miongoni mwa wananchi kuhusu chanjo na washugulikie pia shaka na shuku kutoka kwa wazazi.

Idadi kubwa ya magonjwa yanayosababisha vifo yanaweza kuzuilika kwa chanjo na magonjwa hayo ni pamoja na surua, dondakoo, homa ya ini, polio, homa ya manjano na homa ya mafua makali.

Mkurugenzi Mkuu huyo wa WHO amesema kuwa kampuni kubwa za kidijitali zinawajibika kwa watumaiji wake kwa kuhakikisha wanapata taarifa sahihi kuhusu chanjo na afya.

“Itakuwa jambo jema kuona mitandao ya kijamii inashirikiana ili kuongeza wigo wa kuwafikia watu wao,” amesema Dkt. Tedros akisema kuwa, “tunataka wataalamu wa dijitali wachukue hatua zaidi kusambaza ujumbe ya kwamba chanjo zinafanya kazi.”

Dkt. Tedros amesema kuwa “tunataka ubunifu ambao unasaidia kubadili tabia juu ya masuala ya afya ili kuokoa maisha ya wale walio hatarini zaidi. Watoto wengi ambao wazazi wao wanategemea chanjo hivi sasa wanashinda kupata mbinu hizo za kuokoa maisha.”