Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Sudan Kusini sasa ukatili wa kingono basi! Tumeaibika- Waziri Juuk

Baadhi ya wanawake waathirika wa unyanyasaji wa kingono Sudan kusini wakizungumza na viongozi wa Umoja wa Mataifa
UN Photo/Isaac Billy
Baadhi ya wanawake waathirika wa unyanyasaji wa kingono Sudan kusini wakizungumza na viongozi wa Umoja wa Mataifa

Sudan Kusini sasa ukatili wa kingono basi! Tumeaibika- Waziri Juuk

Haki za binadamu

Nchini Sudan Kusini, jeshi limezindua mpango wa utekeleza wa kutokomeza kabisa ukatili wa kingono unaofanywa na askari wa jeshi hilo dhidi ya raia kwenye maeneo yenye mizozo ambapo maafisa wa ngazi ya juu wameahidi kutokomeza vitendo hivyo vilivyoshamiri tangu vita vya wenyewe kwa wenyewe vianze nchini humo mwezi Disemba mwaka 2013. 

Wakati wa uzinduzi wa nyaraka hiyo iliyoandaliwa kwa zaidi ya miezi miwili, maafisa wa  ngazi  ya juu wa jeshi la Sudan Kusini wameapa kutofumbia macho ukatili wa kingono.

Kila kamanda wa ngazi ya juu atakuwa na nakala yake kwa ajili ya kufundishia askari walio chini yake kuhusu uhalifu wa kingono kwenye mizozo ambapo Waziri wa Ulinzi wa Sudan Kusini Kul Manyang Juuk ameelezea masikitiko yake jinsi taifa hilo limeorodheshwa kimataifa kuwa mtekelezaji wa ukatili wa kingono dhidi ya raia wake.

“Hii ni hali mbaya sana na ndio maana tuko kwenye vikwazo vya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na nchi moja moja. Sasa tufanye nini? Njia bora zaidi ni sisi wenyewe tujiwekee vikwazo na pindi jeshi linawekewa vikwazo, nchi inakuwa imechukua hatua. Hatuwezi kupata hata mkopo wa kuendeleza nchi yetu.Na hii ina maana hatuwezi kutekeleza sera zetu.”

Ujumbe wa umoja wa Mataifa nchini Sudan Kusini, UNMISS ambao umekuwa ukishirikiana na makamanda hao wa jeshi la Sudan Kusini kuandaa nyaraka hiyo, una matumaini kuona nchi hiyo ikiondolewa kwenye orodha ya watekelezaji wa ukatili wa kingono. Alain Noudéhou ni Naibu Mwakilishi wa Umoja wa Mataifa nchini humo.

“Mpango huu wa utekelezaji unapatia msisitizo ahadi ya serikali kwenye vipengele vya katiba na wajibu wake kimataifa ikiwemo haki ya uhuru na usalama na haki ya mtu kutoteswa au kufanyiwa vitendo vyovyote visivyo vya kibinadamu au kupewa adhabu zisizo za kiutu.”

Nyaraka hii ya utekelezaji dhidi ya ukatili wa kingono ni mafanikio ya taarifa ya pamoja iliyotolewa mwaka 2014 na Rais Salva Kiir na Umoja wa Mataifa katika kushughulikia ukatili wa kingono kwenye maeneo ya mizozo nchini humo.