Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNIMISS Imelaani vikali ukatili wa kingono dhidi ya wanawake 125 Bentiu

Wanawake na watoto wa Sudan Kusini wakiwasili katika kambi iliyoko Bentiu humo humo nchini mwao.
UNICEF/Sebastian Rich
Wanawake na watoto wa Sudan Kusini wakiwasili katika kambi iliyoko Bentiu humo humo nchini mwao.

UNIMISS Imelaani vikali ukatili wa kingono dhidi ya wanawake 125 Bentiu

Haki za binadamu

Ujumbe wa  Umoja wa Mataifa nchini Sudan kusini UNMISS umelaani vikali  mfululuzo wa mashambulizi ya ukatili wa kingono dhidi ya wanawake na wasichana waliokuwa wakisafiri kutoka vijijini kwao kuelekea Bentiu kwenye jimbo la Unity.

Takriban wanawake na wasichana 125 wamepatiwa matibabu baada ya kubakwa au kufanyiwa ukatili wa kingono katika muda wa siku 10 wakati wakitembea kwenye barabara za karibu na Nhialdu na Guit wakiwa njiani kuelekea Bentiu. 

Kwa mujibu wa UNMISS waliripoti kuwa ukatili huo ulifanywa na waliokuwa wamevalia mavazi ya kiraia au sare za kijeshi. Na wamesema mbali ya kufanyiwa ukatili wa kingono au kubakwa walipigwa vibaya na kuporwa.

Akizungumzia unyama huo mwakilishi maalumu wa Umoja wa Mataifa nchini Sudan kusini na mkuu wa UNMISS David Shearer amesema“Mashambulizi haya dhidi ya raia wasio na hatia na wasiojiweza ni ukatili usiokubalika na ni lazima yakome.Ukatili huo umefanyika katika maeneo yanayodhibitiwa na serikali na inawajibu wa kwanza wa usalama wa raia. UNMISS imefanya mikutano ya dharura na serikali na kuitaka kuchukua hatua mara moja kulinda wanawake na wasichana katika eneo hilo na kuhakikisha wahusika wa uhalifu huu wa kinyama wanawajibishwa.”

Mwakilishi huyo maalumu ameongeza kuwa “Walinda amani wa UNMISS wamepeleka mara moja askari wa kushika doria katika eneo hilo  kili kutoa ulinzi na timu yetu ya haki za binadamu wameanza uchunguzi ili kubaini wahusika. Wahandisi wa UNMISSwanasafisha majani barabarani ili iwe vigumu kwa washambuliaji kujificha.”

Mpango huo wa Umoja wa Mataifa pia umevitaka vikosi vyote katika eneo hilo kuhakikisha vinadhibiti askari wake ili kuhakikisha askari hao wa ngazi zote hawashiriki katika vitendo hivi vya kihalifu.