Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Maonesho ya sanaa yatumika kumtetea mwanamke, Sudani Kusini.

Maonesho ya sanaa yaliyofanyika Juba nchini Sudan Kusini yakiwa yamefadhiliwa na  ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini  humo,  UNMISS kuelimisha jamii kuhusu jinsia na ukatili wa kingono.
UNMISS\Nektarios Markogiannis
Maonesho ya sanaa yaliyofanyika Juba nchini Sudan Kusini yakiwa yamefadhiliwa na ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini humo, UNMISS kuelimisha jamii kuhusu jinsia na ukatili wa kingono.

Maonesho ya sanaa yatumika kumtetea mwanamke, Sudani Kusini.

Haki za binadamu

Kwa udhamini wa ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Sudani Kusini (UNMISS), wanafunzi wa Sanaa wamefanya maonesho ya kukuza uelewa kuhusu unyanyasaji wa kingono na kijinsia katika nchi yao ambayo imeghubikwa na vita kwa takribani miaka sita sasa. 

Maonesho hayo ni ya kufikisha ujumbe na pia kubadilishan uzoefu kuhusu changamoto zinazowakabili wanawake kwenye migogoro kama  Sudan Kusini. Sarah Aba Afari ni Polisi wa Umoja wa Mataifa katika kitengo cha jinsia, watoto na ulinzi wa raia walioko hatarini.

“Wanafunzi, baadhi ya washiriki au wageni katika warsha hii walikuwa wanauliza kwa nini haya yanatokea? Kwa nini watu wawafanyie vurugu wanawake? Vitendo hivi vinapaswa kukoma. Na wengine walikuwa wanasema haya mambo ni ya kweli kwasababu yanatokea katika jamii zetu na wengine wamewashauri wenzao kuwa tunapaswa kuyaacha haya. Tunahitaji kuacha, si mazuri kwetu. Kwa hivyo maonesho yanakuza uelewa kwa watu wa Sudan Kusini, watu wa aina zote, na hali zote.”

Wanafunzi wanasema sanaa ni njia nzuri ya kuwasiliana kwa kutumia picha katika maeneo ya nchi yenye viwango vya juu vya watu wasiojua kusoma. David Solomon ni mwanafunzi msaani wa Sudan Kusini anaeleza kuhusu picha aliyoichora akisema, “inahusu mfumo wa mahakama za kijadi. Unaweza kuona, katika njia ya kimila, wazee wako hapo, wanaweza kuhukumu kesi dhidi ya wanawake, hususani kama kuna mwanamke, watamlaumu, hawaruhusu mwanamke kuwa kuwa sehemu ya mchakato. Unaweza kuona katika mchoro, wanawake wamekaa mbali sana, na kila mwanamke anapoletwa katika mahakama ya kijadi, wanamlaumu na ndiyo maana mikono yote imeelekea kwa mwanamke. Hawasikilizi haki za manamke na maamuzi ya mwanamke yanapuuzwa katika picha hii. Kwa hivyo ujumbe ninaoupitisha hapa ni kuwa wanawake wanapaswa kushirikishwa katika kufanya maamuzi yoyote.”

Wanafunzi wengi wanapata shida kulipa ili kuingia katika vyuo vikuu katika nchi hii ambayo ni maskini lakini maonesho haya yanawasaidia kuendelea na masomo yao, ambapo nyingi kati ya kazi 50 zinazooneshwa tayari zimeuzwa kwa wapenzi wa kazi za sanaa.

Kwa UNMISS, maonesho ni fursa ya kuwafikia wanafunzi 8,000 kutoka katika makabila na malezi tofautitofauti na pia maelfu ya watu kutoka kwenye jamii ambao wanategemewa kuyatembelea maonesho haya. Na pia ni kuwapatia sauti manusura wa unyanyasaji wa kingono.