Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mahakama ya kuhamahama yapeleka haki Malakal, Sudan Kusini.

Kituo cha Umoja wa Mataifa cha kulinda Raia, Wau, Sudan Kusini.
UN
Kituo cha Umoja wa Mataifa cha kulinda Raia, Wau, Sudan Kusini.

Mahakama ya kuhamahama yapeleka haki Malakal, Sudan Kusini.

Sheria na Kuzuia Uhalifu

Kwa zaidi ya kipindi cha siku tatu, mahakama ya kuhamahama inayofadhiliwa na ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Sudan Kusini, UNMISS, imekuwa katika mji wa Malakal  jimbo la Upper Nile nchini Sudan Kusini ili kushughulikia kesi kadhaa zikiwahusisha watu ambao walitenda makossa makubwa yakiwemo kesi mbili za unyanyasaji wa kingono na moja ya unyanganyi kwa kutumia silaha.

Mjini Malakal, jimbo la Upper Nile, maafisa wa sheria wamesafirishwa kwa njia ya anga kutoka mji mkuu wa Sudan Kusini, Juba kuja kusikiliza kesi ambazo zimesubiri muda mrefu haki kutendeka.

Baada ya kila kitu kuwa kimewekwa katika eneo lake, watuhumiwa wanaletwa kutoka katika vituo vya ulinzi vya Umoja wa Mataifa na wanaingizwa kizimbani huku waliohudhuria wakisubiri maamuzi.

Katika siku ya kwanza kesi ya kijana mwenye umri wa miaka 16 ya ubakaji inatajwa ikifuatiwa na unyang’anyi kwa kutumia silaha.

Siku ya pili ni kesi ya unyanyasaji wa kingono dhidi ya mtoto wa kike mwenye umri wa miaka minne. Mtuhumiwa ni mwanauume mwenye umri wa umri wa miaka 26 mkazi wa kituo cha ulinzi wa raia cha Umoja wa Mataifa Malakal. 

Jaji Marrow Deng wa Mahakama Kuu ya Sudan Kusini baada ya kusikiliza kesi, anatangaza hukumu,

(Sauti ya Judge Marrow Deng)

“Albino Simon Omot unahukumiwa, mosi, kwenda gerezani kwa kifungo cha miaka mitatu kuanzia leo tarehe 21 Februari 2019. Pili, polisi wa Umoja wa Mataifa watakukabidhi kwa mamlaka za magereza za serikali. Hukumu hii imetolewa chini ya usimamizi wangu katika mahakama ya kuhamahama leo tarehe 21 Februari 2019.”

Cecilia Anuar Kac, mama wa mtoto aliyenajisiwa amefarijika,

(Sauti ya Cecilia Anuar Kac)

“Nimefurahi hukumu ilipotangazwa kwa kuwa sheria imechukua mkondo wake.”

Pande zote mbili ule wa mashitaka na washitakiwa wameridhika. Daud Othon Othow wa upande wa mashitaka anasema

(Sauti ya Daud Othon Othow)

“Mtuhumiwa Albino Simon Omot, kesi yake ya jinai ilikuwa chini ya kifungu 396 kuhusu unyanyasaji wa kingono wa umri wa miaka minne. Lilikuwa ni kosa kubwa sana na kuhukumiwa miaka mitatu ana bahati lakini hii itakuwa funzo kwa wale wanaotaka kufanya makosa kama haya.”

Umoja wa Mataifa unasema hii ni mara ya pili haki imekuja Malakal kwa njia ya ndege na magurudumu, mahakama ya kwanza ya kuhamahama ilifika eneo hili tarehe 16 na 20 Oktoba 2018.