OCHA yawaenzi wahudumu wa misaada waliouawa Borno mwaka jana.

1 Machi 2019

Leo ni mwaka mmoja  kamili tangu shambulizi ya kusitikisha kukatili maisha ya wahudumu watatu wa misaada ya kibinadamu kwenye mji wa Rann jimbo la Borno nchini Nigeria.

Akikumbuka mchango wa wahudumu hao mratibu wa masuala ya kibinadamu wa shirika la Umoja wa Mataifa na kuratibu misaada ya kibinadamu na masuala ya dharura OCHA , Edward Kallon amesema wahudumu hao Dkt. Izuogo Anthony Onyedikachi, Emmanuel Yawe Sonter na Ibrahim Lawan walifanya kazi katika mazingira magumu vijijini Kaskazini Mashariki mwa Nigeria karibu na mopaka wa Cameroon wakijitolea kuokoa Maisha ya maelfu ya wakimbizi wa ndani.

Mauti yaliwafika wahudumu hao wakati wa shambulio la Machi Mosi 2018 na kuacha mshangao mkubwa kwa jumuiya ya kimataifa ya misaada, Umoja wa Mataifa na mashirika mengine yasiyo ya kiserikali.

Bwana Kallon amesema “Kila wakati ambapo ghasia zinakatili Maisha ya watu wasio na hatia inatuathiri sote, lakini zaidi inapotupokonya Maisha ya vijana wenye ujuzi na kipaji cha kujitolea kuokoa Maisha ya wenzao maelfu, hilo ni pigo ambalo linagusa kitovu cha utu wetu.”

Wakati wa shambulio hilo makundi yenye silaha yasihusiana na serikali yaliwateka pia wanawake watatu wahudumu wa misaada aambapo Hussaini Ahmed Khorsa na Hauwa Mohammed Liman, wote walikuwa ni wauguzi wakunga na waliuawa na watekaji wao mwezi Septemba na Oktoba2018  na Alice Lokshah, muuguzi na mama bado anashikiliwa hadi sasa.

Umoja wa Mataifa leo mwaka mmoja baada ya tukio hilo unaendelea kutoa wito wa muuguzi huyo kuachiliwa mara moja na kurejeshwa salama kwa familia yake.

Kallon amesema “siku ya leo ni ya hisia mchanganyiko za huzuni na majonzi kwa kila mtu kwenye jumuiya ya misaada ya kibinadamu lakini pia ni ya kukumbuka na kuenzi kujitolea kwao, ujasiri wao na huduma yao ya bila kuchoka na jambo muhimu katika kuwaenzi wahudumu haw ani kuendelea na kazi waliyokuwa wakiifanya kwa kuzingatia misingi ya kibinadamu .”

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud