Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wakimbizi Borno Nigeria walazimika kufungasha virago tena kufuatia shambulio: OCHA

Picha ya UN
OCHA/Franck Kuwonu
Picha ya UN

Wakimbizi Borno Nigeria walazimika kufungasha virago tena kufuatia shambulio: OCHA

Amani na Usalama

Mamia ya watu ambao tayari walizihama nyumba zao kutokana na machafuko Kaskazini Mashariki mwa Nigeria, wamelazimika kufungasha virago tena baada ya mashambulizi yaliyokatili maisha ya watu kadhaa kwenye kambi walizokuwa wanaishi na kwenye jamii zinazowazungunga, imesema ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kuratibu masuala ya kibinadamu na misaada ya dharira, OCHA.

Katika taarifa iliyotolewa leo mbele ya waandishi wa habari mjini Geneva Uswis na msemaji wa shirika hilo Bwana. Jens Laerke” Katika mashambulizi hayo kundi la watu wenye silaha limewauwa watu 8 na kujeruhi wengine wengi, kuteka wanawake, kuchoma na kupora nyumba, makazi na akiba ya chakula.”

Kwa mujibu wa OCHA shambulio hilo limetokea Jumatano wiki hii katika kituo kinachoendeshwa na serikali kilometa chache kutoka Maiduguri, mji mkuu wa jimbo la Borno na katika jamii za karibu na kijiji cha Dalori.

Kambi hiyo ni maskani ya watu 12,600 waliokimbia mapigano katika miezi michache iliyopita ambayo yalikuwa kati ya vikosi vya serikali na wapiganaji wenye itikadi kali ambayo tayari wameshakatili maisha ya watu 29,000 tangu mwaka 2009 na kusababisha moja ya migogoro mikubwa kabisa ya kibinadamu duniani.

Image
Wahudumu wa afya katika kambi ya wakimbizi wa ndani Nigeria. Picha: WHO

Shambulio la juma hili limewafurusha mamia ya watu kwa mujibu wa OCHA na wengi hawajulikani waliko. Shirika hilo limetoa witio kwa serikali kuhakikisha kwamba  jamii za watu wasiojiweza wakiwemo wakimbizi zinalindwa.

Laerke amesisitiza kwamba “Ni wito wa kuongeza juhudi za ulinzi kwa raia jimboni Borno na pia kwenye majimbo mengine mawili , lakini zaidi Borno ambako ndio kitovu cha watu kutawanywa na zahma ya kibinadamu.”

Mbali ya kambi iliyoshambuliwa juma hili kuna kambi zingine 8 za wakimbizi wa ndani maeneo jirani  ambazo ujenzi wake ulianza 2015 , na hivi sasa zinahifadhi watu Zaidi ya 47,000. Na kuna takribani mashirika 20 ya misaada yanayotoa chakula, maji, usafi, madawa na malazi lakini mahitaji bado ni makubwa katika sehemu kubwa ya Kaskazini Mashariki mwa Nigeria.