Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Miaka 10 baada ya kuzuka machafuko Nigeria zahma ya kibinadamu inaendelea:OCHA

Wasichana ambao walikuwa wametekwa na kubakwa na Boko Haram nchini Nigeria.
© UNICEF/UN0126512/Bindra
Wasichana ambao walikuwa wametekwa na kubakwa na Boko Haram nchini Nigeria.

Miaka 10 baada ya kuzuka machafuko Nigeria zahma ya kibinadamu inaendelea:OCHA

Amani na Usalama

Ikiwa ni miaka 10 tangu kuzuka kwa machafuko Kaskazini Mashariki mwa Nigeria Umoja wa Mataifa na wadau wengine wa wa misaada wanasema mahitaji ya kibinadamu yanaendelea kuongezeka na kuyatimiza ni changamoto kubwa.

Wadau hao wa masuala ya kibinadamu ukiwemo Umoja wa Mataifa, mashirika yasiyo ya kiserikali, wawakilishi wa serikali, shirika la kitaifa la masuala ya dharura NEMA , na mashirika mengine ya misaada ya kibinadamu wamekutana leo ili kuadhimisha miaka 10 tangu kuanza kwa machafuko ,lakini pia kuwakumbuka mamilioni ya watu walioathirika na machafuko hayo.

Katika kumbukumbu hiyo shirika la Umoja wa Mataifa la kuratibu masuala ya kibinadamu OCHA limesema jumuiya ya masuala ya kibinadamu inasisitiza kuhusu mahitaji makubwa ya kibinadamu yaliyopo Kaskazini Mashariki mwa Nigeria na ulazima wa kuendelea kuongeza msaada wa kibinadamu kwa mamilioni ya watu hasa kwenye majimbo matatu yaliyoathirika zaidi ya Borno, Adamawa na Yobe. Na pia kuendelea kufanyakazi pamoja kuwasaidia watu hao sio tu kuweza kuishi bali pia kujenga upya maisha yao na jamii zao.

Akizungumza katika kumbukumbu hiyo mratibu wa masuala ya kibinadamu wa Umoja wa Mataifa Nigeria  Edward Kallon amesema “Mgogoro huo ulioanza miaka 10 iliyopita hauna dalili yoyote ya kumalizika, tuko hapa kuwakumbuka wale walipoteza maisha yao na wanaoendelea kuteseka kwa ajili ya machafuko hayo. Huu sio wakati wa kusuasua ni kipindi muhimu sana , lazima tuongeze mara mbili juhudi zetu za msaada katika ngazi zote za kitaifa na kimataifa”.

Katika muongo huo mmoja wa vita raia 27,000 wamepoteza maisha, maelfu kujeruhiwa na pia kusambaratisha jamii, vijiji na miji hususan katika majimbo matatu yaliyoathirika zaidi.

Naye Rais wa mtandao wa mashirika ya misaada yasiyo ya kiserikali NGO’s Nigeria Josephine Habba amesema “Ni muhimu kutoa kipaumbele katika mahitaji na haki za watu hususan wanawake na watoto na kuyawezesha mashirika ya kijamii ili yasaidie zaidi, huu ni mgogoro wa nchi nzima na hatutaki uendelee kwa miaka mingine 10.

Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa mgogoro huo wa Kaskazini mashariki mwa Nigeria ni miongoni mwa migogoro mibaya zaidi duniani ukiwaacha watu milioni 7.1 wakihitaji msaada wa kuokoa maisha na kuwalazimisha wengine milioni 1.8 kufungasha virago na kuzikimbia nyumba zao na waathirika wakubwa ni wanawake na watoto.