Dola milioni 848 zahitajika kunusuru wakimbizi wa ndani kaskazini-mashariki mwa Nigeria

11 Januari 2019

Nchini Nigeria, Kuongezeka kwa mapigano kati ya vikosi vya serikali na makundi yaliyojihami kaskazini mashariki mwezi uliopita wa Desemba na kumesababisha watu wengi zaidi kufurushwa makwao kutoka eneo la Baga na kuelekea kwenye kambi za wakimbizi wa ndani hujo Maiduguri na Manguno ambako tayari  kuna msongamano. John Kibego na taarifa zaidi.

Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kuratibu misaada ya kibinadamu, OCHA, inasema mwaka 2018 zaidi ya watu 214,000 walifurushwa, hususan wanawake na watoto.

Zaidi ya yote  kushamiri kwa mapigano kati ya pande mbili hizo tangu  mwezi Julai kumesababisha  wafanyakazi wa misaada 260  kuhamishwa na hivyo kukwamisha usambazaji wa misaada ya dharura kwa watu 390,000. Jens Laerke ni msemaji wa OCHA mjini Geneva Uswisi na amewaeleza waandishi wa habari hii leo kuwa...

“Umoja wa Mataifa na wadau wanashirikiana na serikali kuwasilisha mahitaji muhimu kwa watu walioko hatarini kabisa wakilenga makazi, chakula, maji na vifa vya kujisafi. Msongamano katika kambi ya “Teachers Village” Maiduguri umeleta  changamoto kwa sababu zaidi ya wakimbizi 20,000 wamewasili katika kipindi cha wiki tatu pekee. Watu hao hawawezi kwenda kambi zingine kwa hofu ya usalama wao.”

Watu zaidi ya milioni 7.1 wanahitaji msaada wa kibinadamu katika majimbo yaliyoathirika ikiwemo Borno, Adamawa na Yobe huku wanawake na watoto wakijumuisha asilimia 80 ya watu walio na mahitaji.

Kwa mujibu wa OCHA, watu 823,000 wamekwama katika maeneo yaliyo vigumu kufikia.

Mpango wa 2019 wa misaada ya kibinadamu inalenga watu milioni 6.2 na unahitaji dola milioni 848.

 

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter