Hatua zichukuliwe kuwalinda wenye ulemavu wa ngozi Malawi:UN

8 Februari 2019

Wataalamu wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa wametaka hatua zaidi zichukuliwe kulinda watu wenye ulemavu wa ngozi nchini Malawi baada ya mtu mmoja mwenye ulemavu wa ngozi kuuawa na mtoto mwenye umri wa mwaka mmoja kutoweka. 

Hofu ni kwamba matukio hayo yanaweza kuongezeka wakati huu ambapo Malawi inaelekea uchaguzi mkuu. Wameitaka serikali kuongeza kasi ya uchunguzi wa matukio hayo na kuwafikisha mbele ya sheria wahusika.

Kwa mujibu wa wataalam hao tangu mwaka 2014 kumekuwa na visa 150 vya mauaji, mashambulizi na ukiukwaji mwingine wa haki za binadamu dhidi ya watu wenye ulemavu wa ngozi nchini Malawi.

Wataalam hao wametoa wito kwa serikali “kushughulikia haraka mizizi ya mashambulizi hayo na kuimarisha kampeni zanchi nzima kuelimisha jamii, kuendesha uchunguzi wa kina na kuzichukulia hatua kesi zote, kuongeza ulinzi kwa waathirika na kufadhili na kutekeleza hatua zote za lazima.”

Licha ya hatua mbalimbali za kuwasaidia watu wenye ulemavu wa ngozi mashambulizi ya karibuni wataalam hao wanasema yanaonyesha kwamba serikali inahitaji kuongeza mara mbili juhudi zake za kukomesha mauaji na ukatili unaoendelea dhidi ya watu hao.

Mashambulizi haya ya karibuni yamefanyika wakati ambapo watu wa Malawi wanajiandaa kwa uchaguzi mkuu uliopangwa kufanyika Mei 2019.

Wakiwa na hofu kwamba uchaguzi huo huenda ukaongeza visa wamesema “Wakati wa uchaguzi unaweza kuwa wa hatari kwa watu wenye ulemavu wa ngozi kwani wakati huu ndio mauaji na mashambulizi huongezeka kwa sababu ya imani potofu kwamba viungo vya watu wenye ulemavu wa ngozi vinaweza kuleta bahati na madaraka vikitumiwa katika ushirikina.”  

Na kuongeza kuwa vitendo vya ukatili vinavyohusiana na ushirikina vinasababisha ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu kama vile mateso, mauaji, ubaguzi, na unyanyapaa ikiwemo kutimuliwa katika jamii.

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud