Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Askari wa kukodiwa ni tishio barani Afrika, tuchukue hatua- Guterres

Katibu Mkuu wa UN António Guterres akihutubia Baraza la Usalama la wakati wa mkutano kuhusu jinsi askari mamluki wanavyotisia usalama na utulivu barani Afrika
UN / Evan Schneider
Katibu Mkuu wa UN António Guterres akihutubia Baraza la Usalama la wakati wa mkutano kuhusu jinsi askari mamluki wanavyotisia usalama na utulivu barani Afrika

Askari wa kukodiwa ni tishio barani Afrika, tuchukue hatua- Guterres

Amani na Usalama

Hoja ya askari mamluki na harakati zao barani Afrika imejadiliwa leo kwenye Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa wajumbe wakiangazia ni kwa jinsi gani askari hao wanatishia siyo tu amani na usalama duniani bali pia uhuru na mamlaka ya mataifa barani humo.

Akihutubia mkutano huo ulioongozwa na Rais Teodoro Obiang Nguema Mbasogo wa Equatorial Guinea ambaye nchi yake ndio inashika kiti cha  urais wa Baraza  la Usalama la Umoja wa Mataifa kwa mwezi huu wa Februari, Katibu Mkuu Antonio Guterres amesema askari mamluki wakijulikana pia askari wa kukodiwa ni suala ambalo limekuwepo enzi na enzi na kutokana na kufanyika kisiri, inakuwa vigumu kupata takwimu.

Athari za askari wa kukodiwa

Hata hivyo amesema ripoti zinadokeza kuwepo kwa ongezeko la matumizi ya askari hao na wapiganaji wa kigeni hali inayofanya mizozo kuzidi kuwa migumu kutatua akiongeza kuwa, “baadhi ya askari mamluki wanahama kutoka vita moja hadi nyingine, wakitekeleza majukumu yao kwa uthabiti mkubwa, bila uwajibikaji wowote na kupuuza kabisa sheria za kimataifa za kibinadamu.”

Akiangazia zaidi Afrika ambayo ndio hoja ilijikita zaidi kwenye mkutano wa leo, Bwana Guterres amesema shughuli za mamluki zinatia hofu kubwa akisema vile ambavyo wanahusika huko ukanda wa Sahel pamoja na kudaiwa kuchochea ghasia baada ya uchaguzi nchini Cote d’Ivoire mwaka 2010.

Guterres amesema askari wa kukodiwa pia wameripotiwa kujaribu kupindua serikali ya Equatorial Guinea na hivyo ametaja mambo matatu ya kuwezesha kukabiliana na askari hao wa kukodiwa barani Afrika.

Hatua tatu kukabiliana na askari mamluki:

  • Kuimarisha mifumo ya kisheria, kitaifa na kimataifa ya kudhibiti askari hao akitolea mfano mkataba wa kimataifa wa mwaka 1989 dhidi ya kuajiri, kutumia, kufadhili na kufundisha askari wa kukodiwa.;International Convention against the Recruitment, Use, Financing and Training of Mercenaries.
  • Kuongeza ushirikiano wa pande mbili, kikanda na kimataifa ikiwemo kwenye usimamizi wa mipaka huko Afrika ya Kati ambako silaha na wapiganaji wa kigeni wanamiminika na kuchochea mizozo. 
  • Kuchunguza sababu za kisiasa, kiuchumi, kijamii na kisaikolojia zinazochochea kuimarika kwa shughuli za askari wa kukodiwa. Juhudi zaidi za kuweka fursa kwa vijana zitakuwa ni jambo jema katika kupunguza vitendo vya vijana kuvutiwa na mamluki na pia kuwa na misimamo mikali. Tuchukue hatua zaidi pia kuwezesha wanawake.
Mwenyekiti wa kamisheni  ya AU Moussa Faki Mahamat wakati akihutubia Baraza la Usalama hii leo kwa njia ya video kwenye mkutano kuhusu mamluki barani Afrika
UN/Cia Pak
Mwenyekiti wa kamisheni ya AU Moussa Faki Mahamat wakati akihutubia Baraza la Usalama hii leo kwa njia ya video kwenye mkutano kuhusu mamluki barani Afrika

Muungano wa Afrika nao wapaza sauti

Mwenyekiti wa Kamisheni ya Muungano wa Afrika, AU Moussa Faki Mahamat amehutubia mkutano  huo kwa njia ya video kutoka Addis Ababa nchini Ethiopia, akisema kuwa licha ya juhudi za kimataifa za kudhibiti askari mamluki bado wanaendelea kutishia serikali za Afrika akitolea mfano wa jaribio la kupindua serikali ya Equitorial Guinea miezi kadhaa iliyopita, jaribio ambamo askari wa kukodiwa walitajwa kuhusika.

Ametilia msisitizo hoja ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ya kusimamia zaidi utekelezaji wa mkataba wa kimataifa wa dhidi ya kuajiri, kutumia, kufadhili na kufundisha askari wa kukodiwa.

Kampuni binafsi za ulinzi za kigeni zatajwa

Bwana Mahamat akaangazia pia kampuni binafsi za ulinzi za kigeni akisema kuwa bila shaka vyombo hivi ni vya kisheria vikifanya kazi kwa ushirikiano na serikali katika kuimarisha usalama.

Hata hivyo amesema uwepo wao na utitiri wao unaanza kutia shaka akisema hivi sasa kamisheni ya AU inaandaa mfumo wa kusimamia na kuratibu kampuni hizo.

Teodoro Obiang Nguema Mbasogo, Rais wa Jamhuri ya Equatorial Guinea ambaye nchi  yake ni Rais wa Baraza la Usalama mwezi huu wa Februari, akihutubia Baraza hilo wakati wa kikao kuhusu vitisho vya amani na usalama duniani, wakimulika zaidi askari wa kukodi
UN/Cia Pak
Teodoro Obiang Nguema Mbasogo, Rais wa Jamhuri ya Equatorial Guinea ambaye nchi yake ni Rais wa Baraza la Usalama mwezi huu wa Februari, akihutubia Baraza hilo wakati wa kikao kuhusu vitisho vya amani na usalama duniani, wakimulika zaidi askari wa kukodi

Askari mamluki wamejaribu mara 5 kupindua serikali ya  Equatorial Guinea nahata kutaka kuniua- Rais Mbasogo 

Akiwa mmoja wa manusura wa harakati za mamluki, Rais  Teodoro Obiang Nguema Mbasogo wa Equatorial Guinea akihutubia mkutano huo amesema nchi yake imekuwa kivutio cha mamluki miaka ya 90 baada ya kugundulika kwa mafuta nchini humo.

“Ni kwamba katika kipindi cha miaka 24, nchi yangu imekuwa manusura wa matukio 5 ya askari wa kukodiwa kuendesha harakati zao kwa lengo la kupindua serikali na hatimaye kujinufaisha na rasilimali za nchi na hivyo kuwanyima wananchi matunda ya nchi yao,” amesema Rais Mbasogo akiongeza kuwa “watu hawa walifanya vitendo vibaya ikiwemo mashambulizi ya benki, kushambulia makazi ya Rais na mwezi Desemba mwaka 2017 walifanya hata jaribio la kuniua mimi na familia yangu yote.”

Kwa mantiki hiyo amesisitiza mshikamano kuondokana na askari hao ambapo naye amerejelea umuhimu wa utekelezaji wa mkataba wa kimataifa dhidi ya kuajiri, kutumia, kufadhili na kufundisha askari wa kukodiwa ambao nchi  yake tayari imetia saini pamoja na mkataba wa Muungano wa Afrika wa kutokomeza askari mamluki barani Afrika wa mwaka 1977 sambamba na maazimio mengine ya Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa.

Ainisho la askari mamluki liangaliwe upya- Rais Paul Kagame

Wajumbe pia walisomewa hotuba ya Rais Paul Kagame wa Rwanda ambaye hivi sasa ndiye mwenyekiti wa Muungano wa Afrika, AU.

Hotuba hiyo imesomwa kwa niaba yake na Waziri wa Mambo ya Nje wa Rwanda, Richard Sezibera ambaye amemnukuu Rais Kagame akitaka ainisho jipya la maana ya mamluki kwa kuzingatia kuwa suala hilo lina historia ndefu Afrika na hutishia uhuru, mamlaka na mipaka ya nchi wanachama.

Hatuwezi na katu hatupaswi kuchelewa kuchukua hatua sahihi- Rais Paul Kagame, Mwenyekiti AU

Amesema mwaka 1977 wakati huo, uliokuwa Umoja wa nchi huru za Afrika OAU, sasa AU, ulipitia mkataba wa kutokomeza mamluki Afrika, wakati huo mamluki wakijulikana kuwa watu walioajiriwa ndani au nje ya nchi kwa lengo la kupigana ili wapate fedha au mali.

“Hata hivyo ainisho hilo hivi sasa haliwezi kutosha kuelezea mamluki. Ni muhimu kutofautisha watoa huduma za ulinzi wanaofanya kazi ndani ya nchi kihalali na vikundi vya mamluki ambavyo vinafanya kazi kisiri na kupatia msaada vikundi vilivyojihami ambavyo vinalenga kutikisa mamlaka halali za nchi,” amesema Rais Kagame.

Halikadhalika amesema mamluki hivi sasa hawahusiki na mapigano pekee bali pia kuna mashambulio ya mtandao na ushushushu viwandani ambao unanufaisha mamluki.