UN na AU zaonyesha wasiwasi kuhusu mwelekeo wa dunia hivi sasa

9 Julai 2018

Umoja wa Mataifa, UN na Muungano wa Afrika, AU wameelezea wasiwasi wao mkubwa juu ya sintofahamu inayoendelea kukumba mfumo wa dunia na kusababisha madhara kwenye amani na usalama duniani.

Katibu Mkuu wa UN Antonio Guterres na Mwenyekiti wa kamisheni ya AU Moussa Faki Mahamat wamesema hayo katika taarifa yao ya pamoja waliyoitoa mwishoni mwa mkutano wa pili wa kila mwaka wa vyombo hivyo viwili mjini Addis Ababa nchini Ethiopia hii leo.

Wamesema kila nchi inapaswa kuzingatia mifumo, misingi na kanuni za kimataifa iliyowekwa kwa lengo la kuimarisha amani na usalama.

Kwa mantiki hiyo Bwana Guterres na Bwana Mahamat wametaka kuimarishwa zaidi kwa mfumo wa kuzuia mizozo kwa kushughulikia visababishi vya mizozano sambamba na kuimarisha michakato ya kisiasa na kuzingatia utawala wa kisheria na mifumo jumuishi ya maendeleo.

Majeshi ya Afrika yaliyoko Sahel yanapambana na magaidi ambao ni tishio kwa dunia nzima.

Mkutano huo pia umetathmmi changamoto za amani, usalama na maendeleo barani Afrika ukigusia hali ya amani kwenye mataifa kadhaa ya Afrika yakiwemo Burundi, Jamhuri ya Afrika ya Kati, bonde la ziwa Chad, Comoro, Sudan Kusini na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

Washiriki wa mkutano huo wa AU-UN  “wamekubaliana kwa pamoja kuongeza usaidizi wao kwa ushirikiano wa karibu na jamii za kikanda kwa ajili  ya amani, usalama na maendeleo pamoja na kuangazia harakati za kuleta utulivu kwenye nchi hizo huku wakiangazia michakato ya kisiasa.Hata hivyo wamesihi hatua za kina za jamii ya kimataifa katika kupunguza majanga ya kibinadamu na hatari hasa kwa jamii zilizo kwenye hatari zaidi.

ULINZI WA AMANI

Katibu Mkuu wa UN na Mwenyekiti wa kamisheni ya AU wamejadili pia mpango wa hatua za utekelezaji kuhusu ulinzi wa amani ambao unalenga kuwezesha operesheni za ulinzi wa amani kuendana na changamoto za sasa ikiwemo katika bara la Afrika.

Bwana Guterres akafafanua zaidi changamoto za operesheni  hizo alipozungumza na waandishi wa habari akisema..

“Lakini kama ilivyokuwa kwa AMISOM na sasa kikosi cha kundi la nchi 5, G5 huko Sahel, vile ambavyo operesheni hizi zimekuwa zikitekelezwa zamani hazikupata msaada wa kutosha kutoka jamii ya kimataifa. Tunahitaji kuimarisha amani Afrika, kukabili ugaidi Afrika kwa kutumia vikosi vya Afrika lakini zikiwa na mamlaka dhahiri na kwa maoni yangu, chini ya ibara ya 7 ya  katiba ya UN na kwa fedha zinazotabirika, yaani fedha kutoka michango ambayo imepangwa.”

Akaenda mbali akisema kuwa 

“Tunapaswa kuelewa kuwa majeshi ya Afrika yanayopambana na magaidi Sahel, hawalindi wakazi wa Sahel pekee, bali wanalinda dunia nzima. Dunia inapaswa kuwa na mshikamano na Afrika, kwa kuwa majeshi ya Afrika yanatulinda sote. Tutashikamana na Muungano wa Afrika kuhakikisha amani na usalama barani Afrika vinasalia kipaumbele cha jumuiya nzima ya kimataifa.”

Viongozi hao wa AU na UN pia “wamepongeza jitihada za kuhuisha misimamo ya kisiasa ya AU na UN ambako operesheni za ulinzi wa amani zinapelekwa kama ilivyodhihirishwa wakati wa ziara ya pamoja ya hivi karibuni ya Mkuu wa operesheni za ulinzi wa amani za UN na kamishna wa amani na usalama wa AU huko Sudan na Jamhuri ya Afrika ya Kati,” imesema taarifa hiyo ya pamoja.

UHUSIANO WA ETHIIOPIA NA ERITREA

Bwana Guterres pia aliulizwa na waandishi wa habari kuhusu uhusiano wa hivi sasa kati ya Ehitopia na Erietria nchi ambazo zimekuwa mahasimu kwa takribani miongo miwili ambapo asema, “naamini kuwa mabadiliko ya sasa ya uhusiano kati ya Eritrea na Ethiopia ni ishara muhimu sana ya matumaini, siyo tu kwa nchi mbili hizo bali pia kwa Afrika na dunia nzima kwa ujumla.”

Amesema pindi jamii ya kimataifa inaposhuhudia mizozo mingi na kushuhudia jinsi nchi mbili hizo kwa miaka mingi zimekuwa kwenye mzozo na kushindwa kuwa pamoja, ni habari njema kuwa utashi wa kisiasa wa  nchi hizo kutatua mzozo kati yao ni Dhahiri.

Katibu Mkuu amesema Umoja wa Mataifa uko tayari kufanya lolote lile ambalo pande mbili hizo zitaomba ufanye ili kumaliza mvutano kuhusiana na mpaka akisema ni wazi kuwa sasa zimeamua kusaka suluhu ya matatizo yao.

Wamekubaliana kuwa mkutano ujao wa AU na UN utafanyika jijini New York, Marekani mwaka 2019.

 

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud