Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Makubaliano  ya amani CAR yatiwa saini Bangui, ni baada ya kupitishwa Khatroum, Guterres azungumza

Wananchi wakiwa na bendera ya Jamhuri ya Afrika ya Kati nchini mwao.
MINUSCA
Wananchi wakiwa na bendera ya Jamhuri ya Afrika ya Kati nchini mwao.

Makubaliano  ya amani CAR yatiwa saini Bangui, ni baada ya kupitishwa Khatroum, Guterres azungumza

Amani na Usalama

Hii leo  huko Jamhuri ya Afrika ya Kati, CAR, wajumbe wa serikali na vikundi 14 vilivyojihami wametia saini makubaliano ya amani yaliyofikiwa kati ya pande mbili hizo mjini Khartoum nchini Sudan mwishoni mwa wiki iliyopita.

Hafla hiyo imefanyika kwenye Ikulu ya nchi hiyo iliyoko mji mkuu Bangui na kuhudhuriwa na Mwakilishi wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini humo Parfait Onanga Anyanga, Rais wa CAR FAustin Archange Touadera na Mwenyekiti wa Kamisheni ya Muungano wa Afrika, AU, Moussa Faki Mahamat.

Akizungungumza wakati wa hafla hiyo, Bwana Onanga Anyanga ambaye pia ni mkuu wa ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kuweka utulivu nchini CAR, MINUSCA amesema, “makubaliano  ya amani ambayo mmeyatia saini, yamefikiwa baada ya kila upande kujitolea kwa mambo mengi. Mkataba unasisitiza maadili ya CAR ambayo yanaruhusu wananchi kuishi vyema pamoja kwa usawa, udugu, haki, maridhiano na kupatia fidia manusura wa mzozo uliokuwepo.”

Kwa upande wake, mwenyekiti wa kamisheni ya AU Bwana Mahammat amesema umuhimu wa makubaliano hayo ni  ushirikishwaji wa pande zote wakiwemo wananchi na ndio maana walitaka utiaji saini ufanyike mjini Bangui na zaidi ya yote ni vyema kuhakikisha mapigano yanasitishwa.

Na hatimaye, Rais Touadera  akasisitiza ushiriki wake katika kutekeleza makubaliano hayo akisema, "tumefanikiwa kujenga makubaliano  ya kihistoria. Sitowasaliti watu wangu. Nitaweka juhudi zangu zote kuhakikisha mkataba wa amani uliokamilishwa huko Khartoum na kutiwa saini Bangui, unatekelezwa. Natoa wito kwa mara nyingine tena kwa pande zilizotia saini makubaliano haya ili tushirikiane kwa  pamoja kukomesha mapigano. Kwa pamoja tumesoma ukurasa wa kitabu kichungu kilichoandika historia  yetu kwa maandishi.  Leo natoa wito tushirikiane kuandika kwa maandishi ya dhahabu ukurasa mpya wa taifa leo kwa pamoja.”

Nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati, CAR, ujumbe wa Umoja wa Mataifa MINUSCA unatekeleza mradi wa matokeo ya haraka ya kuwezesha jamii kupata kipato na kujinusuru na umaskini.
UN/MINUSCA - Hervé Serefio
Nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati, CAR, ujumbe wa Umoja wa Mataifa MINUSCA unatekeleza mradi wa matokeo ya haraka ya kuwezesha jamii kupata kipato na kujinusuru na umaskini.

KATIBU MKUU GUTERRES AZUNGUMZA

Kufuatia kutiwa saini kwa makubaliano hayo, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ametoa taarifa yake ya kupongeza pande husika kwa  hatua hiyo aliyosema ni ya mafanikio makubwa.

Amepongeza dhima ongozi ya Muungano wa Afrika kwenye mazungumzo hayo ambayo yalifanyika pia kwa msaada wa Umoja wa Mataifa chini ya muundo wa AU wa amani na maridhiano CAR.

Katika taarifa iliyotolewa leo na  msemaji wake mjini New York, Marekani, Katibu Mkuu amesihi pande husika kuzingatia ahadi zao za utekelezaji wa makubaliano hayo.

Katibu Mkuu amesisitiza utayari wa Umoja wa Mataifa kusaidia CAR katika kipindi hiki muhiu, na ametoa wito kwa nchi jirani , mashirika ya kikanda na wadau wa kimataifa kusaidia hatua za kijasiri za taifa hilo ili hatimaye liweze kujenga amani ya kudumu pamoja na utulivu.

HALI ILIVYOKUWA YA CAR

CAR imekuwa na mzozo tangu mwaka 2012, kutokana na mapigaon kati ya kikundi cha anti-Balaka chenye waumini wengi wa kikristo, na waasi wa kikundi cha Seleka ambao wengi wao ni waislamu, mzozo huo umesababisha vifo vya maelfu ya watu. Mzozo umesababisha raia wawili kati ya watatu kuwa wategemezi wa misaada ya kibinadamu. Mwaka 2013, vikundi vilivyojihami viliteka mji mkuu Bangui na kusababisha Rais wa wakati huo, François Bozizé akimbie nchi hiyo. Baada ya kipindi kifupi cha kupungua kwa ghasia, mwaka 2015 na uchaguzi ulifanyika mwaka 2016 lakini ghasia zikaanza tena mwishoni mwa mwaka huo huo.