Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Zaidi ya watoto 30 wapoteza maisha Syria kutoka na ghasia na mazingira magumu

Machafuko yanayoendelea tangu Disemba 2018 yamewalazimisha maelfu ya watu kuzikimbia nyumba zao, miji na vijiji vyao wilayani Hajin Mashariki mwa Deir-ezZor, Syria. Familia zimefunga safari ndefu na ya dhiki kusaka usalama kwenye kambi ya Al-Hol
©UNICEF/ Syria 2019/ Delil Souleiman
Machafuko yanayoendelea tangu Disemba 2018 yamewalazimisha maelfu ya watu kuzikimbia nyumba zao, miji na vijiji vyao wilayani Hajin Mashariki mwa Deir-ezZor, Syria. Familia zimefunga safari ndefu na ya dhiki kusaka usalama kwenye kambi ya Al-Hol

Zaidi ya watoto 30 wapoteza maisha Syria kutoka na ghasia na mazingira magumu

Amani na Usalama

Ghasia, ukimbizi wa ndani na mazingira magumu nchini Syria vimesababisha takribani watoto 32 kufariki dunia tangu mwezi Disemba mwaka jana.

UNICEF kupitia taarifa yake iliyotolewa leo mjini New York, Marekani, imesema mapigano yasiyokoma kwenye maeneo yanayozingira eneo la Hajjin, mashariki mwa Syria, yamelazimu watu kufanya safari ndefu na ngumu ili kusaka usalama kwenye kambi ya al-Hol

Kambi hiyo ya wakimbizi wa ndani iko kilometa zipatazo 300 kaskazini mwa Syria ambapo yaelezwa tangu mwezi uliopita, takribani watu 23,000 wengi wao wakiwa ni wanawake na watoto wamewasili kwenye kambi hiyo.

Hata hivyo wanawasili baada  ya siku tatu wakipitia mazingira magumu kama vile jangwani huku baridi kali ikiwapiga na wao  hawana mavazi au vifaa vya kujikinga na hali hiyo ya hewa.

Familia 400 zimepata hifadhi katika kituo cha makazi ya muda huko Idlib nchini Syria na watoto nao wamepata fursa ya kusomea kwenye mahema
© UNICEF/Aaref Watad
Familia 400 zimepata hifadhi katika kituo cha makazi ya muda huko Idlib nchini Syria na watoto nao wamepata fursa ya kusomea kwenye mahema

“Ukosefu wa usalama umesababisha wahudumu wa kibinadamu washindwe kuwafikia watoto hao na kwamba mazingira magumu safarini  na katika vituo vya ukaguzi ambapo familia wakati mwingine hutumia siku tatu, yamesababisha watoto wapatao 29 kufariki dunia, 11 kati yao wakiwa ni watoto wachanga waliofariki dunia siku mbili zilizopita pekee,” imesema taarifa hiyo ya UNICEF.

Ni kwa mantiki hiyo UNICEF inasaidia watoto na mama zao ambao wanakimbia mji wa Hajjin kwa kuwapatia blanketi, maji safi na salama vifaa vya kujikinga na baridi kali, huduma za afya na lishe pamoja na vituo rafiki kwa watoto sambamba na kuunganisha watoto na familia zao.

Halikadhalika inatoa msaada huo huko Idlib kwa kushirikiana na wadau wake ambapo UNICEF inatoa wito kwa pande zote kuwezesha na kufanikisha ufikishaji wa mahitaji yote ya msaada wa kibinadamu kwa watoto.

Shirika hilo limekumbusha kuwa pande kwenye mzozo nchini Syria zimepuuza sheria za kivita na hivyo linatoa tena wito kwa pande hizo kuhakikisha usalama wa watoto kwenye maeneo yote ya mozo na kwamba hakuna kisingizio chochote kwa kuwa watoto si walengwa wa vita na katu hawapaswi kulengwa.