Watoto 12 wauawa Syria katika wiki mbili zilizopita

4 Mei 2019

Takribani watoto 12 wameuawa kaskazini-magharibi mwa Syria tangu tarehe 20 mwezi uliopita wakati huu ambapo ghasia zinazidi kwenye ukanda ambao haupaswi kuwa na mapigano.

Hiyo ni kwa mujibu wa Mkurugenzi Mtendaji wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF, Henrietta Fore kupitia taarifa iliyotolewa leo na shirika hilo mjini New York, Marekani.

Bi. Fore amesema kando ya kuuawa kwa watoto hao, zaidi ya watu 30,000 wamefurushwa makwao kutokana na ghasia hizo za  mwezi Aprili.
 
Amesema miundombinu ya kijamii nayo imeathirika akisema kuwa “vituo vine vya afya havifanyi kazi baada ya kushambuliwa na kusambaratishwa na kuacha maelfu ya watu bila huduma za afya za kuokoa maisha yao.”

Bi. Fore amesema shule nazo zimeshambuliwa na kuharibiwa huko Idleb na Hama akiongeza kuwa mapigano yalishamiri zaidi siku mbili zilizopita na kusababisha, “wadau wetu walioko kwenye maeneo hayo wasitishe mipango yao ya kusambaza maji safi na salama, huduma za kujisafi. Takribani watu 5,500 hawana kabisa maji. Huduma hizi zitarejea pindi hali ya usalama itakapoimarika.”
 
Mkurugenzi Mtendaji huyo wa UNICEF amesema, “timu zetu zinafanya kazi kwa ushirikiano na wadau kusambaza huduma muhimu lakini iwapo mapigano hayatakoma hakuna la ziada tunaloweza kufanya.”

Amesema kwa mara nyingine wanasihi pande kinzani kwenye mzozo wa Syria ulioingia mwaka wa nane sasa na wale walio na ushawishi nao walinde watoto.

“Kuua au kuacha watoto na ulemavu ni ukiukwaji mkubwa wa haki za watoto. Miundombinu ya kijamii ikiwemo vituo vya afya, maji, elimu nayo haipaswi kulengwa na katu isishambuliwe,” amehitimisha Bi. Fore kwenye taarifa hiyo ya UNICEF.

 

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter