Waisraeli waliowashambulia wapalestina wawajibishwe-OHCHR
Ofisi ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa, OHCHR imesikitishwa na vurugu za mashambulizi ya muda mrefu dhidi ya wapalestina ikirejelea shambulizi la hivi karibuni katika kijiji cha Al Mughayyir kilichoko katika ukingo wa magharibi wa mto Jordan.
Taarifa iliyotolewa hii leo na msemaji wa ofisi ya haki za binadamu mjini Geneva Uswisi Rupert Colville imesema kuwa katika shambulizi hilo la tarehe 26 Januari ya mwaka huu wa 2019 mpalestina mmoja mwenye umri wa miaka 38 baba wa watoto wanne, Hamdi Taleb Na’asan alipigwa risasi mgongoni na kuuawa.
Akielezea tukio hilo, Rupert Colville amesema “maafisa wetu wanasema mauaji yalifanyika katika ukingo wa magharibi baada ya kundi la takribani walowezi 30 wa kiisraeli baadhi yao wakiwa wamejihami na silaha wakitokea eneo la karibu la nchini Israel Adei Ad walipowavamia wakulima wa kipalestina katika mashamba yao na kisha wakaingia katika Kijiji ambako walitumia silaha za moto kuwapiga risasi wanakijiji na nyumba zao”
Colville amesema mashambulizi hayo yalisababisha wanakijiji sita kupigwa risasi za moto na watatu kati yao walijeruhiwa sana.
Msemaji huyo wa OHCHR ameongeza kuwa ingawa vikosi vya usalama vya Israeli vilikuwa karibu na Kijiji na kwa haraka walifahamishwa kuhusu shambulizi hilo, mashuhuda waliiambia wafanyakazi wa ofisi ya haki za binadamu waliotembelea Kijiji hicho jana kuwa iliwachukua saa mbili kwa vikosi vya usalama kuingilia kati na hata vilipoingilia kati vilitumia mabomu ya machozi kuwasambaratisha wanakiji wapalestina.
Wapalestina wengine watatu walijeruhiwa baada ya vikosi vya usalama vya Israeli kuingilia kati ijapokuwa haijafahamika waliowajeruhi ni wavamizi au askari. Jumla wanakijiji 20 walijeruhiwa katika tukio hilo.
OHCHR imesema kwa mujibu wa sheria za kimataifa, Israeli inatakiwa kuwalinda wapalestina dhidi ya mashambulizi hayo na wale waliohusika naa tukio hilo wanatakiwa kuwajibishwa.