Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Huku misaada ikipungua, mwaka wa 2018 umeshudia ongezeko la majeruhi kwa wapelestina: OCHA

Baadhi ya nyumba za  mtaa wa Shejaiya Gaza zilizoharibiwa na mlipuko wa bomu na ikiwa haina maji wala umeme.
UNICEF/El Baba
Baadhi ya nyumba za mtaa wa Shejaiya Gaza zilizoharibiwa na mlipuko wa bomu na ikiwa haina maji wala umeme.

Huku misaada ikipungua, mwaka wa 2018 umeshudia ongezeko la majeruhi kwa wapelestina: OCHA

Amani na Usalama

Kwa mujibu wa ofisi ya Umoja wa Mataifa inayoratibu misaada OCHA, kwa mwaka huu wa 2018, vikosi vya Israel vimewauwa wapalestina 295 na kuwajeruhi wengine zaidi ya 29,000, hii ikiwa ndiyo idadi kubwa ya vifo kuwahi kutokea kwa mwaka mmoja tangu mgogoro wa Gaza uanze mwaka 2014 na pia kuwa na idadi kubwa ya majeruhi tangu tangu OCHA ianze fuatilia majeruhi katika eneo la Palestina linalokaliwa, maarufu kama oPt.

OCHA imetoa takwimu hizi hii leo mjini Gaza, Palestina katika ripoti ya mukhtasari wa yale waliyokusanya katika kipindi cha mwaka mzima wa 2018 katika eneo hilo.

Taarifa hiyo inaendelea kufafanua kuwa takriban watu 180 sawa na asilimia 61 waliofariki, asilimia 79 majeruhi ambao ni zaidi ya watu 23,000 walikuwa katika maandamano ya Gaza katika ukuta wa sengenge. Wapalestina 57 waliokufa, na majeruhi 7,000 walikuwa wenye umri ulio chini ya miaka 18. Takribani wapalestina 28 waliouawa na vikosi vya Israel mwaka wa 2018 walikuwa wanachama wa makundi yenye silaha sehemu za Gaza huku wengine 15 wanadaiwa kuchochea mashambulio dhidi ya Israel katika eneo la Ukingo wa Magharibi.

Kwa upande wa Israel, ripoti inasema, kwa ujumla raia wake 14 waliuawa na wa palestina katika kipindi hicho na wengine takriban 137 walijeruhiwa. OCHA inasema kuwa ingawa idadi ya waliofariki inakaribia kama ya mwaka uliotangulia wa 2017, watu 15, lakini idadi ya raia wa kawaida waliofariki iliongezeka  ikilinganishwa na ile ya mwaka wa 2017. Mwaka uliopita vifo vilikuwa asilimia 27 ilhali mwaka 2018 vilikuwa asilimia 50.

Upatikanaji wa chakula nao ni mgumu mjini aza kutokana na umaskini, usalama mdogo na ukosefu wa ajira.
WFP/Wissam Nassar
Upatikanaji wa chakula nao ni mgumu mjini aza kutokana na umaskini, usalama mdogo na ukosefu wa ajira.

Pia OCHA imeorodhesha visa vya mashambulizi ya raia kwa raia wa pande zote.

Katika mwaka wa 2018 OCHA imeorodhesha visa 265 ambapo walowezi wa Israel waliua ama kujeruhi wapalestina au kuharibu mali ya wapalestina. Idadi ya visa hivyo mwaka 2018 ilikuwa juu hadi kufikia asilimia 69 ikilinganishwa mwaka wa 2017 ambapo mwanamke mmoja wa Kipalestina aliuawa na wapalestina wengine 115 kujeruhiwa. Miongoni mwa mali za wapalestina zilizoharibiwa na walowezi wa Israel ni: miti 7,900 na magari takriban 540.

Mwaka 2018, watawala wa Israel walibomoa ama kuchukua kwa nguvu majengo 459 ya wa Palestina eneo la Ukingo wa magharibi, sanasana katika eneo la C na Jerusalem Mashariki, kwa kukosa vibali vya kujenga ambavyo vimetolewa na Israel, ambavyo ni vigumu kuvipata.

Visa kama hivyo vimewafanya wapalestina 472, wakiwemo watoto 216 na wanawake 127 kukosa makazi. OCHA inasema idadi hii ni ndogo tangu ianze kurekodi hatua za kuyabomoa makazi mwaka wa 2009.

Katika eneo C kuna majengo zaidi ya 13,000 yanayosubiriwa kuvunjwa pamoja na shule kadhaa, OCHA inasema.

Ripoti ya OCHA pia imegusia suala la uhaba wa fedha za kugharimia shughuli za utoaji misaada ya kibinadamu. Inasema kuwa mbali na kuwa mahitaji ya msaada wa kibinadamu yakiwa yaliongezeka mwaka wa 2018, kiwango cha ufadhili kimepungua mno. Ni dola milioni 221 tu ambazo zimepatikana  kati ya zote dola milioni 540 zilizohitajika mwaka mzima wa 2018.

Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa, tafadhali jisajili na pia unaweza kupakua apu ili kuweza kusikiliza wakati wowote popote ulipo.