Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Aibu ya kurejea nyumbani mikono mitupu inatuponza:Wahamiaji 

Taswira kupitia dirisha la chuma ikionyesha mazingira ya wahamiaji waliolala kwenye magodoro sakafuni kwenye moja ya vituo vya kushikilia wahamiaji nchini Libya
UNICEF/Romenz
Taswira kupitia dirisha la chuma ikionyesha mazingira ya wahamiaji waliolala kwenye magodoro sakafuni kwenye moja ya vituo vya kushikilia wahamiaji nchini Libya

Aibu ya kurejea nyumbani mikono mitupu inatuponza:Wahamiaji 

Wahamiaji na Wakimbizi

Vijana wengi kutoka barani Afrika ambao huchagua njia ya uhamiaji usio wa kawaida, ni kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo ukweli mkwamba mustakabali wao uko njiapanda na hawana matumaini mengine ya maisha kwa mujibu wa utafiti uliofanya na shirika la Umoja wa Mataifa la mpango wa maendeleo UNDP.

Huyo ni mmoja wa wahamiaji kutoka Afrika aliyejaribu kwenda kusaka maisha bora barani Ulaya na lakini hali ilipomshinda akarejea nyumbani anasema… vijana wengi tunadhani Ulaya ni peponi lakini hilo si sahihi.

Kwa UNDP ambayo imeendesha utafiti maalum kwa nchi mbalimbali barani Afrika kwa ajili ya kuwasaidia wahamiaji hawa ujulikanao kama “scaling fences” inasema wahamiaji hawa kutoka Afrika hasa vijana ambao wengine ni wasomi wanaamua kufungasha safari hizo na kuwa wahamiaji Ulaya kwa lengo moja tu la kusaka fursa bora za maisha kwa kuwa Afrika haziko.

Huko wanakumbana na mitihani mingi na hata mateso lakini kurudi nyumbani inakuwa vigumu. Seraophine Wakana ni afisa wa UNDP nchini Gambia “Unapokwenda na ukashindwa kufanikiwa una uhakika kwamba ukirudi familia itakuwa imesikitishwa sana.”

Wahamiaji ambao wamerejeshwa pwani ya Libya baada ya kufunga safari kupitia bahari kuelekea Ulaya wakipokelewa na wafanyakazi wa IOM.
IOM Libya
Wahamiaji ambao wamerejeshwa pwani ya Libya baada ya kufunga safari kupitia bahari kuelekea Ulaya wakipokelewa na wafanyakazi wa IOM.

Familia, ndugu, jamaa na marafiki waliowaacha nyumbani wanakuwa na matarajio makubwa na unaposhindwa kuyafikia basi ni aibu si kwako tu kwa familia nzima. Massandje kutoka Corte D’voire alijaribu kwenda Ulaya lakini akaishia Libya na kurudi nyumbani mikono mitupu " Mimi sikuona aibu kurejea kwa maana sikukopa hata senti ya mtu hapa wala kule , nilijihangaikia mwenyewe na sasa nimerudi na nimeleelewa kuwa mambo mengi tunayoyafikiria kumbe sio. "

Seraphine anaongeza kuwa fikra kama hizo za na matarajio na hasa kwa waliosalia Afrika pia zinachangia sana kwa wahamiaji kuona bora wateseke waliko kuliko kurejea nyumbani

“Mara zote wanafikiri kwamba ukiwa Ulaya unatengeneza pesa na wanastahili kupokea fedha hizo kutoka kwako na wakipata chochote na kukuona unarejea nyumbani na pengine uko katika hali ya kuhitaji msaada kutoka kwao, inakuwa ngumu, si rahisi kwa jamii kukubali hali hiyo. Na hii inaweza kuwa funzo kwa wale ambao wanawasukuma watoto wao kwenda kwingine.”

Wahamiaji na wakimbizi kutoka nchi tofauti wakiwasili kwa treni maalumu katika mji wa Berlin Ujerumani
UNICEF/Ashley Gilbertson VII
Wahamiaji na wakimbizi kutoka nchi tofauti wakiwasili kwa treni maalumu katika mji wa Berlin Ujerumani

Chioma ni miongoni mwa vijana wahamiaji ambaye sasa anaishi Ulaya na amekuwa akisaidia kupokea baadhi ya Waafrika wanaofika kusaka maisha  kama alivyofanya yeye,  ana ujumbe mmoja tu kwa wahamiaji kutoka Afrika “Msione aibu kusema ukweli , ukweli utaweza kusaidia kuokoa maisha . Kwa nini unaona haya kwa sababu unataka kutoa taswira ambayo si ya kweli? Wakati kaka zetu na dada zetu wanakufa Libya, wakati kaka zetu na dada zetu wanabakwa, wanazama baharini?wakati wanawekwa rumande na kwenye hospital za vichaa? Tunaweza kuzuia yote haya endapo tutaipa kisogo aibu na kusema ukweli.

UNDP inasema dhamira kubwa ya kuyaweka haya bayana ni kutaka kuonyesha hali halisi inyowakabili wahamiaji kutoka Afrika na kuzichagiza serikali za bara hilo kuhakikisha inakidhi matakwa ya vijana ili wasigeukie safari hizo za hatari.