Elimisha zaidi umma kuhusu sayansi ya tabianchi ili raia wapate ufahamu - Wanamazingira Afrika
Elimisha zaidi umma kuhusu sayansi ya tabianchi ili raia wapate ufahamu - Wanamazingira Afrika
Wanaharakati na watetezi wa mazingira wametoa wito kwa wadau kujikita zaidi katika juhudi za kuuelimisha umma kuhusu sayansi ya tabia nchi ili raia wapate ufahamu. Wanamazingira hao wametoa tathmini hiyo jijini Nairobi nchini Kenya wakizungumza na mwandishi wa Idhaa ya Kiswahili ya Umoja wa Mataifa nchini humo Thelma Mwadzaya.
Viongozi wa bara la Afrika wamekutana jijini Nairobi kwa kongamano la siku tatu la masuala ya tabia nchi lililoambatana na wiki nzima ya majadiliano kuhusu suala hilo hilo. Kwenye vikao, wanaharakati wa mazingira na tabianchi wametoa wito ya kwamba pamoja na kusaka ufadhili wa fedha za miradi ya ujenzi wa mnepo, wamulike pia kuelimisha wananchi wa kawaida kuhusu suala zima la mabadiliko ya tabia nchi, mbinu mujarab za kuhimili dhoruba zake na njia za kunufaika.
Sayansi ipatiwe uzito kama ufadhili
Kongamano la wiki nzima la masuala ya tabianchi lilitazamwa kama fursa mwafaka kwa bara la Afrika kuyarai mataifa tajiri yaliyo na viwanda vinavyotoa viwango vikubwa vya gesi za viwanda ambazo zinachagia katika mabadiliko ya tabianchi, kutenga hela za ziada za kuandaa mikakati ya kuhimili dhoruba zake na pia kukumbatia mifumo safi zaidi ya nishati endelevu. Madaraka Katana ni mwanaharakati wa kundi la Kilifi Youth on The Move lililoko pwani ya Kenya na anahisi tamko la viongozi inahitaji kuipa uzito swala la tabianchi kwasababu, “Afrika inahitaji na inataka kupigana na janga la mabadiliko ya tabianchi kwa sababu ni kitu kinachotuathiri kama waafrika.”
Ahadi zitekelezwe
Wafadhili wakuu ambao ni Marekani na Umoja wa Ulaya hawakutoa kauli za msingi kuhusu kutimiza ahadi walizotoa. Hata hivyo, Afrika ina imani kuwa siasa za mazingira huenda zikafua dafu. Waridi Tamu ni mwanaharakati anayetumia sanaa kuwaelimisha vijana kuhusu mazingira na anaamini wanawake wakipewa fursa mabadiliko yataonekana haswa pale ambapo, ”Wanawake wako mstari wa mbele kwa kweli. Ninavyoona wengi walijitokeza na kuna idadi kubwa ya wanawake waliokuwako kwenye mikutano. Wengi waliohudhuria walikuwa wanawake.Kwahiyo wanawake sasa hivi wamehamasishwa kwamba wajisali kwenye makundi ambapo watakuwa wanapokea fedha hasa hasa wale ambao wameathiriwa na mabadiliko ya tabianchi wale ambao wanatokea hizo sehemu kame, sehemu ambazo hazina maji , wengi sasa hivi wamehamasishwa kupitia hili kongamano,” anasisitiza.
Makubaliano ya Paris na COP27
Kongamano la Nairobi limetoa wito wa kuwa na juhudi za pamoja kupunguza gesi za viwanda ili kuwa na uwiano na makubaliano ya Paris kadhalika utekelezaji wa hazina maalum ya kuzinusuru nchi zilizo hatarini na zinazoathiriwa na mabadliko ya tabianchi iliyofikiwa katika kongamano la COP27. Dorcas Naishorua ni mwanamazingira na mwakilishi wa jamii za kiasili zinazopambana na mabadiliko ya tabianchi ana kwa ana na anasisitiza kuwa ipo nuru kwasababu, “Jamii za kiasili mara nyingi husahaulika kwenye shughuli na mazungumzo ya mazingira pia kutangamana na waafrika wengine. Kupitia fursa hii ambayo tumepewa na serikali kuu ya Kenya tumeweza kupata sauti za jamii za asili. Tunapata changamoto hasa kwa maisha ya mtoto wa kike, kukiwa na kiangazi msichana hataweza kwenda shule, yule mama wa msichana akiwa hana hela ya kumnunulia sodo basi maisha yake yataathirika na hili limekuwa jambo linalowatatiza wengi wa jamii za kiasili.”
Soko la hewa ukaa
Kongamano la Afrika la tabianchi lilifikia makubaliano ya jinsi kupambana na athari zake kadhalika uwezo wa kufyonza hewa ukaa ila hakukuwa na maelezo kamili ya jinsi ya kuhimili dhoruba hizo. Lugha iliyotumika kwenye tamko la Nairobi liendelee kuyapa uzito mbinu za kukabiliana au utekelezaji. Viongozi na wadau wanajiandaa kwa mkutano wa COP 28 utakaofanyika UAE mwishoni mwa mwaka huu.