Watoto waweka rehani maisha kuingia Ulaya, chonde chonde wasaidieni- Unicef
Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF limesihi serikali za nchi za Ulaya kukubaliana juu ya mpango wa kikanda wa kulinda watoto wahamiaji na wakimbizi ambao wanaendelea kukumbwa na hatari kubwa na ukiukwaji mkuu wa haki za binadamu wakati wa safari za kuelekea Ulaya na ni pindi wanapowasili barani humo.
Kauli hiyo ya UNICEF imo kwenye taarifa iliyotolewa leo mjini Geneva, Uswiwi wakati huu inaelezwa kuwa takribani watoto 400 wakimbizi na wahamiaji wamewasili kwenye fukwe za Ugiriki, Italia na Hispania wiki mbili za mwanzo za mwezi huu wa Januari.
Hii ina maana kuwa kila siku kwa wastani watoto 29 wameingia Ulaya kuanzia tarehe mosi hadi 15 mwezi huu.
“Watoto wanapitia machungu mengi wakati wa safari hiyo ya kuvuka bahari ya Mediteranea hasa ikizingatiwa kuwa sasa ni msimu wa baridi kali,” imesema taarifa hiyo ikinukuu ripoti za mwishoni mwa wiki ambapo kat iya watu 170 wanaoohofiwa kufa maji baharini Mediteranea, miongoni mwao ni watoto na mjamzito mmoja.
Taarifa imeenda kwa kina ikisema, “wiki iliyopita, mtoto wa kike mwenye umri wa miaka 9 kutoka Iraq, aliripotiwa kufa maji kwenye bahari ya Mediteranea wakati akijaribu kufikia kisiwa cha Samos yeye na familia yake.”
Kama hiyo haitoshi, mapema mwaka huu takribani watoto 6 walikwama wakiwa kwenye boti ya uokozi ya Sea Watch kwasababu boti hiyo haikuwa ina kibali cha kutia nanga na walisalia humo kwa siku 18 hadi kibali kilipopatikana.
Mkurugenzi wa UNICEF kanda ya Ulaya, Asia ya Kati ambaye anahusika pia na masuala ya uhamiaji Afshan Khan amesema, “kila siku watoto wanaweka rehani maisha yao kusaka usalama na fursa za kujenga mustakabali wenye hadhi. Mfumo wa kikanda utasaidia kuzuia watoto hawa kukumbwa zaidi na ukatili ambao wameshakabiliana nao kwenye safari zao za kusaka maisha bora.”
UNICEF inasema mipango zaidi ya uhamiaji inayopatia kipaumbele watoto inahitajika kwenye nchi zaidi za Ulaya sambamba na mipango ya kuunganisha familia.