Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mikakati yoyote kwa wahamiaji Ulaya izingatie haki za watoto- UNICEF

Wahamiaji kutoka kituo walimokuwa wakishikiliwa nchini Libya na kusafirishwa hadi Niger
UNHCR/Jehad Nga
Wahamiaji kutoka kituo walimokuwa wakishikiliwa nchini Libya na kusafirishwa hadi Niger

Mikakati yoyote kwa wahamiaji Ulaya izingatie haki za watoto- UNICEF

Wahamiaji na Wakimbizi

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF limesihi Muungano wa Ulaya, EU,  na wanachama wake kuchukua hatua thabiti, za pamoja na za wakati il kuokoa Maisha ya watoto wakimbizi na wahamiaji kabla hawajaingia barani Ulaya.

Mkuu wa ofisi ya UNICEF kanda ya Ulaya na Asia Afshan Khan amesema hayo katika taarifa iliyotolewa leo mjini Geneva, USwisi wakati huu ambapo viongozi wa EU wanajadiliana suala la mustakhbali wa wakimbizi na wahamiaji wanaosaka hifadhi Ulaya.

“Mfumo wa kuwasili kwa makundi hayo ambao unasimamiwa na umepangwa vizuri utaokoa Maisha ya watoto wengi kabla ya kufika Ulaya na zaidi ya yote utashughulikia shaka na shuku na kutokufahamu hatma yao pindi wanapowasili.

Ametaka vituo hivyo vya kuwasili wakimbizi na wasaka hifadhi ni lazima view vya wazi vikiwapatia mapokezi na mfumo wa haraka wa utambuzi bila kusahau eneo la kuhifadhi watoto na familia zao.

Bi. Khan amesema vituo hivyo viende sambamba na uwekezaji kwenye mifumo ya ulinzi wa watoto pindi wanapowasili.

Wahamiaji wakiwa wamelala kwenye magodoro kwenye moja ya vituo vya kushikilia wahamiaji huko nchini Libya.
UNICEF/Alessio Romenzi
Wahamiaji wakiwa wamelala kwenye magodoro kwenye moja ya vituo vya kushikilia wahamiaji huko nchini Libya.

Amesisitiza kuwa, “katu watoto wasiswekwe ndani kutokana na hadhi yao ya uhamiaji au ya wazazi wao. Watoto wasiokuwa na msindikizaji yeyote lazima wapatiwe mlezi na waunganishwe na familia zao iwapo ni sahihi kufanya hivyo.”

Afisa huyo wa UNICEF amesema maslahi ya mtoto yapatiwe kipaumbele.

Halikadhalika amesema UNICEF inasihi EU na Muungano wa Afrika, AU waazimie kutekeleza mpango ambao kwao watoto watakuwa salama na kwamba viongozi wa vyombo hivyo wasake suluhu za vyanzo vya watu kukimbia nchi zao.

Amesema UNICEF iko tayari kusaidia EU na nchi wanachama katika harakati hizo.