Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Chondechonde, watoto wanahitaji msaada zaidi kutokana na athari za moto-UNICEF Australia

Kikosi cha zima moto huko Queensland, Australia wakipambana na moto mkali
Queensland Fire and Emergency Services
Kikosi cha zima moto huko Queensland, Australia wakipambana na moto mkali

Chondechonde, watoto wanahitaji msaada zaidi kutokana na athari za moto-UNICEF Australia

Msaada wa Kibinadamu

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF nchini Australia limetuma salamu zake za masikitiko kwa watoto na familia zilizoathirika na janga la moto linaloendelea kote nchini Australia.

“Tungependa kutambua kutokuwa na ubinafsi, na pia kitendo cha ueledi na kujitolea kwa waokoaji, kikosi cha zima moto, Msalaba mwekundu wa Australia na mashirika maengine ambao tayari wako katika maeneo wakipambana na moto huo.” Imeeleza taarifa ya UNICEF iliyotolewa jumatatu hii.

Aidha taarifa hiyo imeendelea kueleza namna UNICEF inavyotambua matamanio ya watu kutoka kote duniani wanavyotaka kushiriki katika kusaidia  kwa namna yoyote kuanzia katika wakati huu ambao moto unaendelea n ahata matokeo ya baadaye ya athari za moto huo.

“UNICEF ina utaalamu na uzoefu wa kimataifa wa kukabiliana na dharura ikiwemo majanga ya asili. Kutoka katika miongo ya kufanya kazi na mamilioni ya watu kote duniani, tunafahamu kuwa watoto ndio ambao mar azote ni miongoni mwa watu wanaokuwa hatarini katika mazingira kama haya.” Imesema taarifa ya UNICEF.

Vilevile UNICEF Australia imeeleza kuwa inafahamu kuwa katika katika matkuio kama haya, mchango wa mabadiliko ya tabianchi  unafanya hali kuwa mbaya zaidi. Shirika hilo limetoa mfano wa hivi karibuni katika kuwasaidia watoto na vijana wadogo katika maeneo yaliyoathiriwa na ukame huko New South Wales kulikotokea moto wa nyika.

“Ni muhimu sana kwa watoto ambao wameishi katika majanga kurudi kwenye maisha ya kawaida haraka iwezekanavyo, na njia moja bora ya kufanya hivyo ni kuwasaidia waanze tena masomo.” Imeshauri UNICEF

Aidha UNICEF imetoa wito kwa wadau wa misaada kuhakikisha misaada inakuwepo kwa ajili ya watoto walioathirika na pia wito umetolewa kwa wazazi kuwaelezea watoto kuhusu kile kinachotokea ili wawezei salama.