Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Makubaliano ya Stockholm yameleta matokeo chanya kwa kiasi fulani Yemen- Griffiths

Martin Griffiths (kwenye skrini) akihutubia wajumbe wa Baraza la  Usalama la Umoja wa Mataifa kwa njia ya video kutoka Amman, Jordan leo Januari 9, 2019
UN /Loey Felipe
Martin Griffiths (kwenye skrini) akihutubia wajumbe wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kwa njia ya video kutoka Amman, Jordan leo Januari 9, 2019

Makubaliano ya Stockholm yameleta matokeo chanya kwa kiasi fulani Yemen- Griffiths

Amani na Usalama

Mjumbe maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kwa ajili ya Yemen, Martin Griffiths ameliambia Baraza la Usalama la Umoja huo leo kuwa pande kinzani kwenye mzozo wa Yemen kwa kiasi kikubwa zimezingatia usitishwaji wa mapigano Hudaydah kwa mujibu wa makubalianao yaliyofikiwa mjini Stockholm, Sweden mwaka jana.

Akihutubia baraza hilo kwa njia ya video kutoka Amman, Jordan, Bwana Griffiths amesema uhasama umepungua toka wakati huo, ila “kwa bahati mbaya na pengine katika hali ambayo haishangazi, kumekuwa na ukatili katika baadhi ya maeneo ikiwemo mji wa Hudaydah na katika wilaya za kusini.

Hata hivyo, ameongeza kuwa “hii ni kwa kiwango cha chini ikilinganishwa na kile tulichoshuhudia kabla ya makubalianao ya Stockholm”.

Mjumbe maalum huyo amesema licha ya kwamba utekelezaji umekuwa taratibu lakini kumekuwa na mchango dhahiri kuelekea kufikia amani.

Bwana Griffiths amesihi pande husika kwenye mzozo zisikatishwe tamaa kufikia dhamira yao kwa sababu ya vikwazo vyovyote vitakavyowakumba ambavyo havikutarajiwa na kuliomba baraza hilo lizitie moyo pande hizo husika kwa kushikilia msimamo na kukabiliana na changamoto pamoja watakazokumbana nazo.

Kuhusu hali ya msaada wa kibinadamu, mratibu wa ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kuratibu misaada ya kibinadamu, OCHA Mark Lowcock amesema licha ya makubaliano hayo, “siwezi kusema kuwa hali ya kibinadamu Yemen imeimarika. Inasalia kuwa janga.”

Bwana Lowcock amesema, “zaidi ya watu milioni 24 wanahitaji msaada wa kibinadamu ikiwa ni asilimia 80 ya watu wote ikijumuisha watu milioni 10 walio hatarini ya kukumbwa na njaa.

Kwa upande wake, mwakilishi maalum wa kudumu wa Yemen kwenye Umoja wa Mataifa balozi, Abdullah Ali Fadhel Al-Saadi, ameliambia baraza hilo la usalama kuwa utekelezaji wa makubaliano ya Stockholm kwa kuzingatia muda uliokubaliwa ni muhimu sana.

Ameongeza kuwa, “ni dhahiri kuwa hili linahitajika kufanyika kabla ya mchakato mpya wa majadiliano kuanza.