UN yathibitishwa kusafirishwa kwa wayemen waliojeruhiwa kutoka Sana’a kwenda Oman

3 Disemba 2018

Ofisi ya mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa kwa Yemen imethibitisha kusafirishwa kutoka mji mkuu wa nchi hiyo, Sana’a kwenda Muscat, Oman kwa wayemen 50 waliojeruhiwa.

Kwa mujibu wa ukurasa wa mtandao wa kijamii wa Twitter wa mjumbe huyo, Mark Griffiths, wayemen hao wanapelekwa Oman kwa ajili ya matibabu.

Bwana Griffiths, ameshukuru pande zote ambazo zimesaidia kufanikisha kitendo hicho cha kibinadamu.

Amesihi raia wote wa Yemen washirikiane ili kusaka  amani na utulivu nchini humo.

YEMEN YAJADILIWA GENEVA

Wakati huo huo, kamati ya uratibu wa masuala ya kibinadamu duniani imekuwa na kikao chao huko Geneva, Uswisi hii leo, ikiwa ni kikao chao cha pili cha mwaka chenye lengo la kutathmini changamoto za kibinadamu duniani.

Taarifa ya wajumbe hao ambao wanajumuisha wawakilishi 20 ikiwemo 19 wa mashirika ya Umoja wa Mataifa na mshirika wake, imesema kuwa Yemen ndio ilipatiwa kipaumbele katika majadiliano yao.

“Tunatiwa hofu sana na kuzidi kudorora kwa kasi kubwa kwa hali ya kibinadamu nchini Yemen kwa miezi kadhaa sasa, mamilioni ya maisha ya watu yakiwa hatarini,” imesema taarifa hiyo ikinukuu jumla ya washiriki 20 wa kikao hicho.

WITO KWA PANDE KINZANI YEMEN

Wawakilishi hao wametoa wito wa kusaka mbinu ya kuwa na sitisho la kudumu la mapigano hususan kwenye mji wa  bandari wa Hudaydah.

Wamesema wanachosaka sasa ni usaidizi wa kimataifa kwa ombi la fedha kwa Yemen ili hatimaye waweze kukidhi mahitaji ya walio hatarani zaidi mwaka ujao wa 2019.

Wametumia fursa hiyo pia kutoa wito kwa pande kinzani Yemen kuelekea Sweden kwa ajili ya mazungumzo yanayoitishwa na Bwana Griffiths, na zaidi ya yote washiriki kikamilifu ili wakubaliane juu ya hatua za kuchukua kumaliza sintofahamu ya sasa nchini Yemen.

 

 

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud