Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Shambulio lingine lalenga watoto Yemen, OCHA yapaza sauti

Mvulana nchini Yemen akiwa kwenye chumba cha wagonjwa kwenye hospitali ya Al Joumhouri mjini Sana'a nchini Yemen akisubiri matibabu.
Giles Clarke/UN OCHA
Mvulana nchini Yemen akiwa kwenye chumba cha wagonjwa kwenye hospitali ya Al Joumhouri mjini Sana'a nchini Yemen akisubiri matibabu.

Shambulio lingine lalenga watoto Yemen, OCHA yapaza sauti

Amani na Usalama

Kwa mara nyingine tena ndani ya wiki mbili watoto nchini Yemen wameshambuliwa na kuuawa huko jimboni Hudaydah.

Mkuu wa ofisi ya Umoja wa Mataifa inayohusika na usaidizi wa dharura Mark Lowcock amesema tukio hilo la karibuni zaidi hapo jana lilitokea kwenye wilaya ya Al Durayhimi na kusababisha vifo vya watoto 22 na wanawake wane.

Amesema watu hao walikuwa wanakimbia mapigano kwenye wilaya  hiyo wakati waliposhambuliwa na kombora la kutoka angani.

“Hii ni mara ya pili ndani ya wiki mbili shambulio la angani kutoka ushirika unaoongozwa na Saudi Arabia umesababisha janga miongoni mwa raia,” amesema Bwana Lowcock katika taarifa iliyotolewa leo Ijumaa jijini New York, Marekani.

Amesema kama hiyo haitoshi, watoto wengine wanne waliuawa katika shambulio lingine la anga huko Al Durayhimi hapo jana.

Tarehe 9 mwezi Juni mwaka 2018, mtoto wa kike akiwa anapata matibabu kwenye hospitali ya Althawra jimboni Hudaydah. Alijeruhiwa yeye na kaka yake pamoja na mjomba wake wakati walipokuwa wanajaribu kukimbia mapigano na kumsaka baba yake.
© UNICEF/Kamal Ayyashi
Tarehe 9 mwezi Juni mwaka 2018, mtoto wa kike akiwa anapata matibabu kwenye hospitali ya Althawra jimboni Hudaydah. Alijeruhiwa yeye na kaka yake pamoja na mjomba wake wakati walipokuwa wanajaribu kukimbia mapigano na kumsaka baba yake.

Mkuu huyo wa OCHA ameesma kinachomsikitisha zaidi ni kwamba maeneo ya misaada kibinadamu nayo yanashambuliwa akitolea mfano hospitali na miundombinu ya maji.

Halikadhalika wahudumu wa kibinadamu wanapata shida kufikia wahitaji akisema watu wanapaswa kuwa huru kukimbia mapigano na kusaka misaada ya kibinadamu.

“Narejelea taarifa ya hivi karibuni ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusu Yemen, inayolaani mashambulio ya aina hiyo dhidi ya raia na natoa wito uchunguzi huru, usioegemea upande wowote ufanyike haraka kwa matukio haya ya hivi karibuni zaidi,” amesema Bwana Lowcock.

Bwana Lowcock amesihi pande kinzani nchini Yemen zizingatie wajibu wao kwa mujibu wa sheria za kimataifa za kibinadamu na kwamba wale wenye ushawishi kwa makundi hayo yatumie ushawishi huo kuhakikisha lolote linalowezekana linafanyika ili kulinda raia.

Kwa mujibu wa OCHA, janga la Yemen ndio janga kubwa zaidi la kibinadamu duniani hivi sasa ambapo raia watatu kati ya wanne wanahitaji msaada.

Mwaka huu pekee, Umoja wa Mataifa na wadau wake wamefikishia msaada watu milioni 8 nchini humo.

TAGS: Yemen, Hudaydah, Mark Lowcock