Mashauriano huko Sweden kuhusu Yemen yamezaa matunda- Griffiths

Kutokuelewana kwa muda mrefu kati ya pande zisizokinzana nchini Yemen, kumesababisha uharibifu mkubwa wa maisha na mali.
OCHA/Giles Clarke
Kutokuelewana kwa muda mrefu kati ya pande zisizokinzana nchini Yemen, kumesababisha uharibifu mkubwa wa maisha na mali.

Mashauriano huko Sweden kuhusu Yemen yamezaa matunda- Griffiths

Amani na Usalama

Majadiliano ya kisiasa yaliyoratibiwa na  Umoja wa Mataifa  yakihusisha pande mbili katika mzozo wa Yemen yamewezesha mabadiliko katika baadhi ya masuala, amesema mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa kwa ajili ya Yemen, Martin Griffiths akizungumza na waandishi wa habari nchini Sweden.

Bwana Griffiths amesema kuwa baada ya majadiliano ya siku tano kati ya serikali ya Yemen na wapinzani wahouthi wamezungumzia kufunguliwa kwa uwanja wa ndege kwenye mji mkuu wa Yemen, Sana’a, kupunguza uhasama katika miji ya Taiz na Hudaydah na kubadilishana wafungwa ambapo kwa mujibu wa ripoti za vyombo vya habari, ni takriban majina 15,000 ya wafungwa kutoka pande zote.

Bwana Griffiths amesema hali mbaya ya kiuchumi ni miongoni mwa mambo waliyoyajadili kwani baada ya miaka minne ya mzozo uchumi wa Yemen umesambaratika na kusababisha mzozo wa kibinadamu ambapo watu takriban milioni 8 wako katika hatari ya njaa na zaidi ya robo tatu ya watu wanategemea msaada wa kibinadamu na ulinzi.

Kwa mujibu wa ripoti, Umoja wa Mataifa umependekeza kwamba bandari ya Hudaydah isimamiwe na wahouthi na serikali ya Yemen kwa uangalizi wa Umoja wa Mataifa. Bwana Griffiths amekuwa akitoa msukumo kwa Umoja wa Mataifa kuonogza usimamizi wa bandari ambayo ametaja ka ma njia muhimu ya misaada inayosaidia familia.

Mjumbe huyo ameeleza kutiwa moyo na mtazamo chanya na mzito wa pande mbili husika na kwamba anamatumaini makubwa kuhusu matokeo ya majadiliano akitaja kuwa makubaliano rasmi yatatangazwa baada ya mazungumzo yanayofanyika mjini Stockholm nchini Sweden.

Raia wa Yemen wakiwa katika mstari wa kusubiri msaada wa kibinadamu uliokuwa ukisambazwa na UNICEF katika maeneo ya Hudaydah mwezi juni 2018.
UNICEF
Raia wa Yemen wakiwa katika mstari wa kusubiri msaada wa kibinadamu uliokuwa ukisambazwa na UNICEF katika maeneo ya Hudaydah mwezi juni 2018.

 

Bwana Griffiths amesema, “matumaini ndio kishawishi cha mpatanishi; na iwapo hautaweka mazingira ya kuwa na matumaini, hautawatia watu moyo kujituma zaidi.” Akiongeza kuwa anatarajia kuwa kutakuwa na hatua muhimu katika siku chache zijazo.

Halikadhalika Mjumbe maalum huyo anatazamia majadiliano ya pili ya pande husika  ambayo yanapangwa kufanyika mwakani.

Guterres aelekea Sweden kushiriki mashauriano kuhusu Yemen

Katika hatua nyingine, imeelezwa kuwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ameelekea Sweden ili aweze kushiriki siku ya mwisho ya mashauriano kati ya pande kinzani nchini Yemen.

Mashauriano hayo yanamalizika Alhamisi wiki hii baada ya kuongozwa na mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa kwenye mzozo wa Yemen, Martin Griffiths.

Taarifa ya msemaji wa  Umoja wa Mataifa imeeleza kuwa tangu kuanza kwa mashauriano hayo yaliyoanza tarehe 6 mwezi huu wa Desemba yamejumuisha wawakilishi wa serikali na wale kutoka upande wa wahouthi kwa lengo la kupunguza machungu yanayokumba wayemen na pia kurejesha mchakato wa amani.

Katibu Mkuu atakuwa na mikutano na wajumbe kutoka pande mbili hizo na atazungumza katika kikao cha mwisho cha kufunga mashauriano hayo.