Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mama Katarina ni mfano wa jinsi nishati endelevu inavyobadili maisha-FAO

Mama Katarina na familia yake ambaye tangu kuanza kutumia umeme utokanao na samadi tangu 2012 anatoa mafunzo kwa wanakijiji wenzake.
©FAO/Christabel Clark
Mama Katarina na familia yake ambaye tangu kuanza kutumia umeme utokanao na samadi tangu 2012 anatoa mafunzo kwa wanakijiji wenzake.

Mama Katarina ni mfano wa jinsi nishati endelevu inavyobadili maisha-FAO

Ukuaji wa Kiuchumi

Nchini Tanzania mradi mpya wa shirika la chakula na kilimo duniani, FAO wa kuzalisha umeme kwa kutumia samadi ya wanyama, umekuwa mkombozi kwa wafugaji wa ng’ombe ambao kwa muda mrefu wamejikuta kiwango kikubwa cha maziwa kinaharibika kutokana na ukosefu wa majokofu ya kuhifadhi.

Mradi huo INVESTA unapatia wafugaji na kaya uwezo na ujuzi wa kutengeneza visima vya kuhifadhi mbolea ya mifugo ambayo baadaye baada ya kumeng’enywa na bakteria huzalisha nishati ya ya umeme.

FAO Tanzania inasema kuwa sekta ya maziwa nchini humo ambayo bado haijakua, imekuwa ikikubwa na changamoto kwasababu ni asilimia 12 tu ya lita bilioni 2.5 za maziwa yanayozalishwa nchini humo huwafikia walaji kupitia wafanyabiashara wadogo.

“Takribani asilimia 90 ya kaya za vijijini hazina umeme kwa hiyo wazalishaji maziwa wanashindwa kutunza maziwa wanayokamua ng’ombe jioni hii ikimaanisha kuwa kwa kuwa hawana majokofu ya kuhifadhi, ifikapo asubuhi  yanakuwa yameshaharibika,” amesema Alessandro Flammini, afisa wa FAO nchini Tanzania.

MRADI WA INVESTA

Jawabu kwa wafugaji wadogo wa vijijini na wauzaji wa maziwa ya ng’ombe sasa limepatikana kupitia INVESTA ambao ni mradi wa kuwekeza teknolojia za nishati endelevu kwenye sekta ya kilimo na chakula ambapo FAO Tanzania inashirikiana na bodi ya maziwa nchini Tanzania kupigia chepuo matumii ya mtambo huo wa kuzalisha nishati kwa kutumia samadi au kinyesi cha mifugo.

FAO inasema mtambo huo baada ya kutoa nishati ya umeme, masalia yake ambayo ni madini kama vile Fosforasi na Potasiyamu yanasambazwa kwenye mazao na hivyo kupunguza matumizi ya mbolea zenye kemikali.

MAMA KATARINA NI MFANO

Tayari mradi huo wa INVESTA umezaa matunda na FAO inataja shuhuda wake kuwa ni Mama Katarina ambaye nyumbani wake amefunga mtambo tangu mwaka 2012 na sasa anapata nishati ya kupikia na pia kuhifadhi maziwa.

Mma Katarina sasa anatumia nishjati itokanayo na samadi kwa ajili ya umemem na kwa jiko lake analotumia kupikia familia.
©FAO/Alessandro Flammini
Mma Katarina sasa anatumia nishjati itokanayo na samadi kwa ajili ya umemem na kwa jiko lake analotumia kupikia familia.

“Mama Katarina sasa ni mtaalamu kwenye eneo lake akisaidia kufundisha wanakijiji wengine matumizi ya mtambo huo na faida zake kwa kuwa yeyye hivi sasa mtambo huo unamsaidia kupika mila mitatu ya siku kwa familia yake ya watu 6.

Makala ya FAO inasema kuwa Mama Katarina amehakikisha mtambo wake umeegemezwa vyema ili kuepusha kutwama wakati wa msimu wa mvua na pia umejengwa kiasi cha kuelekea upande wa jua ili kila wakati uwe una joto.

FAO inataja faida kuu tatu za mtambo huo kwa wakulima nchini Tanzania kuwa ni nishati ya kupikia, mbolea ya mazao shambani na mapato yatokanayo na biashara ya maziwa ambayo hayajaharibika.

Shirika hilo linaamini kuwa kupitia FAO INVESTA, wakulima wanapata kipato, wanaweza kuwa na chakula na hivyo kutokomeza njaa na umaskini ifikapo mwaka 2030 kwa kutumia teknolojia hiyo rahisi ya nishati hiyo endelevu.

Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa, tafadhali jisajili na pia unaweza kupakua apu ili kuweza kusikiliza wakati wowote popote ulipo.